>

MUDA WA KAZI NI SASA KWA KILA TIMU KUFANYA KWELI

MAANDALIZI makubwa ambayo yamefanywa na kila timu yanakwenda kutoa picha ya
ushindani kwenye mechi zijazo katika ligi pamoja na mashindano ya kimataifa.

Baada ya nguvu kubwa kuhamia kwenye usajili kisha maandalizi kwa msimu mpya ni muhimu kuongeza nguvu nyingine kwenye maboresho ya viwanja.

Kila mmoja anapenda kile anachokifanya kiwe katika ubora. Ubora wa mpira unabebwa na sehemu ambayo wachezaji watakuwa wanachezea hapo uwanjani, hivyo tu basi.

Sehemu ya kucheza, uwanja ni muhimu sana kufanyiwa maboresho kwa wakati huu ili ligi itakapokuwa inaendelea iwe ni mwendo mdundo mwanzo mwisho.

Zile taarifa kuwa uwanja fulani unafungiwa kwa kuwa hauna vigezo kwa msimu mpya isiwe ni mara kwa mara kwa kuwa maandalizi yanapaswa kuwa bora kila sekta.

Pia zipo timu ambazo zilishindwa kupata matokeo kwenye mechi za nyumbani kwa kuwa hawakuwa nyumbani walichezea ugenini wakiwa nyumbani.

Kucheza nje ya nyumbani hata ukiwa wewe ni mwenyeji uhalisia wa kuwa nyumbani unayeyuka jumlajumla hivyo ni muhimu kuongeza nguvu kwenye maboresho ya viwanja vya nyumbani.

Vikosi ni muhimu kuboreshwa na viwanja pia ni muhimu kuboreshwa kwa kuwa kila idara inategemea kupata matokeo mazuri kwa kutegemeana.

Wachezaji wanapenda kupata matokeo lakini uwanja unaamua matokeo yawe ni ya aina gani kama mazingira hayatakuwa rafiki hapo kila mmoja atakuwa anatafuta sababu.

Bado hatujawa imara kwenye upande wa umiliki wa viwanja kwa kuwa timu chache zinamiliki viwanja bora hivyo ni wakati wa kujipanga kwa umakini kwa msimu mpya kuwa na viwanja
bora.