VIONGOZI FANYENI KAZI YENU ISHU YA UMAARUFU NI WACHEZAJI

    INAWEZEKANA ikawa kama miaka saba au nane iliyopita niliibuka na hoja ya suala la viongozi wanaoingia kwenye mchezo wa soka, kuacha kuutumia kwa sababu ya ndoto zao za kisiasa pekee.

    Niliwaeleza viongozi wa mlengo huo kuwa walikuwa hawafanyi sahihi kwa kuingia kwenye mchezo wa soka, kuongoza kwa lengo la kuja kuwa wabunge au mawaziri hapo baadaye.

    Niliwakumbusha nguvu ya mpira kwa jamii kuwa una nafasi kubwa na kuutumikia kwa ufasaha, basi kwa taifa inaweza kuwa bora wakati mwingine kuliko hata upande wa siasa kwa kuwa mbunge au waziri.

    Nilicholenga ni suala la viongozi wanaokua bora kuacha kuondoka baada ya muda mfupi kwa kuwa tu walitaka kuwa wabunge au kufanya mambo mengi kwa ajili ya faida zao na kujitangaza wao badala ya kuangalia mpira unapata faida gani kupitia wao wakiwa ni viongozi.

    Tunakubaliana sote kuwa uongozi ni dhamana na unapopewa, unakuwa mtumishi wa watu hilo lipo wazi hivyo muhimu ni kutimiza yale ambayo ni haki bila kubagua kwa pande zote.

    Sasa angalia kama umeona mambo vizuri katika kipindi hiki cha misimu mitatu iliyopita, kuna wimbi kubwa la viongozi wa mpira kuamini wao ndio kila kitu katika timu na klabu wanazoziongoza,

    Unakuta kiongozi anataka sifa zote za kocha ziende kwake, utafikiri yeye ndiye amekuwa mazoezini na timu wakati wote au yeye ndiye aliliongoza benchi la ufundi wakati wote na kwa kuwa walishinda basi ndiye anapaswa kupewa sifa hizo.

    Mshambuliaji kaibuka bora, anataka sifa ziende kwake, beki kasifiwa kwa ubora anataka kila kitu apewe yeye.

    Ikitokea kuna rundo la wachezaji walikuja chini ya uongozi wake wameboronga au kuleta hasara kwenye klabu, kiongozi huyo hataki kabisa kuhusishwa na kulijadili suala hilo ni sawa na kumshambulia.

    Angalia kwa upande wa wasemaji kuhusiana na suala kama hilohilo, unaona msemaji au mhamasishaji anaweza akawa anajivunia kama vile ndiye alicheza uwanjani.

    Tena asingependa kusikia wachezaji wakijivunia sana suala la wao kuwa waliotoa mchango mkubwa uliosaidia au kupelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa katika kikosi chao.

    Msemaji huyohuyo, unaweza kusikia akiwasema wachezaji kwa maneno mabaya huku akionyesha hawakufanya lolote baada ya kuondoka na hii inafuta yote waliyoyafanya wakati wakiwa pale.

    Nafikiri tunaweza kukiri kwamba ni kipindi ambacho utandawazi umechukua nguvu kubwa sana lakini tunapaswa kuwa makini na hatua tunazopiga ili kuendana nao ili tusitoke njiani.

    Kwa viongozi wanaotaka kuwania ubunge au ndoto ya kuwa mawaziri, wakumbuke hawapaswi kulazimisha mambo. Kama timu imefanya vizuri, utambuzi wa kazi nzuri ya kiongozi au mkuu au wale wasaidizi, inatambulika. Lakini lazima kuheshimu ubora wa kazi ya kocha au ubora wa kazi ya wasaidizi wake na wachezaji kwa ujumla.

    Kuendelea kutaka kuonyesha kila kitu kimefanywa na mtu mmoja au wawili tu au wale wanaozungumza tu ni jambo baya sana katika afya ya kikosi cha mpira.

    Wachezaji ndio wanaotakiwa kuwa wa kwanza kupata sifa kubwa katika mpira kwa kuwa hii ni field play. Mafanikio yake yanapatikana uwanjani, wanaokwenda kutazamwa ni wale wanaocheza uwanjani na si wale wanaokaa VIP kuwatazama wanaopambana kwa ajili ya timu na heshima ya klabu.

    Inatosha kiongozi ukaongoza vizuri, ukafanya vizuri na kuwaachia watu waamue. Kwani hata ukiwa mbunge, utafanya kazi zako za uongozi na huwezi kulazimisha kuwa mwananchi au watendaji wa kazi zako. Waache wafanye kazi zao vizuri na mwisho sifa itafika kwako yenyewe tu.

    Tubadilike na tuache kuwakandamiza makocha na wachezaji kwa sababu ya ndoto zetu binafsi.

    Previous articleMUHIMU KULINDANA KWA WACHEZAJI HIVYO TU BASI
    Next articleHII HAPA REKODI YA SIMBA MPYA