AMANI ni nkitu cha msingi kwenye kila idara ikiwa ni pamoja na familia ya michezo. Hivi karibuni kwenye matamasha pamoja na mechi za kimataifa tumeshuhudia vurugu.
Utaratibu ambao umekuwa ukitumika, ni miongoni mwa sababu ya mashabiki kuwa sehemu ya vurugu hizo hasa wakati wa kuingia uwanjani.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kuelekea Simba Day, kuwepo mipango makini ambayo itajali afya ya mashabiki pamoja na wachezaji wa mpira.
Kuanzia kwenye upande wa mashabiki, hawa wamekuwa ni wahanga wakubwa kwenye upande wa wale ambao huwa wanakuwa kwenye fujo nyingi.
Ipo wazi kuwa, muda wa kuingia huwa unatajwa na mashabiki wanatambua lakini kwenye mpangilio wa kuingia na mageti ambayo yanafunguliwa imekuwa tatizo.
Kuna mechi moja ya kimataifa, mashabiki wengi walipata maumivu kutokana na kuruka mageti wakiwa kwenye harakati za kuingia uwanjani.
Mwisho, baada ya kuwa kwenye furaha kutokana na mchezo huo, waliishia kupata maumivu yaliyowapelekea kwenda hospitali kupewa matibabu.
Hii ni mbaya kuendelea kutokea kwa mashabiki, hasa wakiwa kwenye harakati za kuiona timu inacheza soka la kupendeza.
Mpira ni burudani na mashabiki wanapenda kuona burudani, hivyo amani ni muhimu kuendelea kudumu kila wakati.
Kama ambavyo sera ya Simba inasema nguvu moja basi iwepo na kwenye utaratibu wa mashabiki kuingia uwanjani pamoja na usimamizi mzuri.
Kwa upande wa wachezaji ni jukumu lao kutambua kwamba mpira ni urafiki na sio uadui mechi za kimataifa za kirafiki hazihitaji nguvu nyingi bali akili na kutumia makosa ya wapinzani.
Ikumbukwe kwamba kuna mashindano mengine yapo njiani ikiwa ni pamoja na ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mashabiki pia ni muhimu kuwa makini kwenye kutimiza majukumuyenu kwa kufuata utaratibu ambao utawekwa na imebainishwa kuwa tiketi zimeisha hivyo kwa ambaye atakuwa amekosa tiketi ni jukumu lake kuwa sehemu salama kwake na sio uwanjani kugombania kuingia ndani.