MAYELE MZEE WA KUTETEMA ‘THANK YOU’

    MZEE wa kutetema Fiston Mayele hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga msimu mpya wa 2023/24 baada ya kupata changamoto mpya ndani ya kikosi cha Pyramids ya Misri.

    Hapa tunakuletea baadhi ya aliyofanya akiwa na uzi wa Yanga namna hii akikutana na Thank You:-

    Tuzo zake

    Ana tuzo ya ufungaji bora ndani ya ligi msimu wa 2022/23 alipotupia mabao 17 akiwa na uzi wa Yanga sawa na kiungo mshambuliaji wa Simba Saido Ntibanzokiza.

    Wote wawili walitwaa tuzo ya ufungaji bora na walitajwa kwenye kikosi bora cha ligi iliyokuwa na ushindani mkubwa.

    Pia nyota huyo ni mchezaji bora, (MVP) msimu wa 2022/23 na tuzo ya bao bora kwenye ligi aliikomba pia na uzi wa Yanga.

    Kwenye anga la kimataifa Yanga iligotea hatua ya fainali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa ni washindi wa pili.

    Mayele alitwaa tuzo ya ufungaji bora alipotupia jumla ya mabao 7 Julai 30 alikutana na Thank You ndani ya Yanga.

    Mvuja jasho

    Alivuja jasho kwenye mechi 26 akikomba dakika 2,028 chini ya Nasreddine Nabi ambaye naye hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga msimu mpya wa 2023/24.

    Mayele alikosekana kwenye mechi nne za ligi kati ya 30 ambazo Yanga ilicheza kwenye ligi huku akiwa hayupo kwenye kumbukumbu ya mwamuzi yeyote Bongo kwenye orodha ya nyota wenye kadi ya njano wala nyekundu.

    Kete ya mwisho

    Kete yake ya mwisho kwa nyota wa Yanga Mayele ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons alitupia bao moja dakika ya 33 akitumia pasi ya Salim Aboubhakari, ‘Sure Boy’.

    Mchezo huo ulikuwa ni wa ligi alipogotea kwenye mechi 26 msimu wa 2022/23 hata kwenye mchezo wa Kombe la Azam Sports Federation ambao ulikuwa wa fainali dhidi ya Azam FC alikosekana kwa kuwa alikuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa.

    Mtibua rekodi

    Rekodi aliyoandika Mayele msimu wa 2021/22 kutupia mabao 16 kwenye ligi aliitibua alipofunga mabao 17.

    Mzawa George Mpole alitwaa tuzo ya ufungaji bora alifunga mabao 17.

    Yeye na Simba

    Simba walipata tabu walipokutana na Mayele kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa Uwanja wa Mkapa katika Ngao ya Jamii kwa kuwatungua mabao mawili.

    Ilikuwa ni Agosti 13 2022 walipokuwa nyuma kwa bao moja lililopachikwa na kiungo Pape Sakho dakika ya 14 aliyetumia pasi ya Clatous Chama.

    Ngoma ilipinduliwa kipindi cha pili na Mayele aliyewatungua Simba dakika ya 49 na 80.

    Baada ya mchezo huo Mayele alisema: “Walipotufunga mapema walishangilia wakijua wameshinda tumeshinda na kombe tumechukua,”.

    Wote wamesepa

    Wafungaji wa mabao kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii 2022/23 wote wamesepa Sakho kauzwa na mabosi wa Simba Ufaransa huku Mayele yeye akiibukia ndani ya kikosi cha Pyramis ya Misri kwa ajili ya changamoto mpya.

    Mayele amekabidhiwa jezi namba 9 ile aliyokuwa akiitumia ndani ya Yanga.

    Yeye na Azam FC

    Mayele alibainisha kuwa miongoni mwa timu ambazo huwa zinakamia kwenye mechi kubwa ni pamoja na Azam FC ilikuwa kwenye mahojiano yake kuelekea katika mchezo wa fainali wa Azam Sports Federation.

    “Azam FC ni timu bora lakini huwa inakamia mechi hivyo tukikutana nao mchezo huwa unakuwa mgumu,”.

    Previous articleNTIBANZOKIZA KWENYE REKODI YAKE BONGO
    Next articleVIDEO:ISHU YA UKARABATI UWANJA WA MKAPA KUTUMIA BILIONI