MAANDALIZI YA MSIMU MPYA YAANZE MAPEMA

    BAADA ya kusimama kwa muda kupisha ratiba ya mashindano ya kimataifa, Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2022/23 ilirejea rasmi Juni 6 Jumanne kwa michezo nane kupigwa kwenye viwanja mbalimbali nchini.

    Kufuatia matokeo ya Juni 6 kila mmoja alianza kuona picha kamili baada ya kesi ya ubingwa kufungwa mapema na Yanga kufanikisha malengo yao.

    Yanga ni mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo na rasmi kwenye mchezo wa Juni 9 walikabidhiwa kombe lao, lakini tayari timu zinazomaliza nafasi nne za juu zimekwishafahamika na zile ambazo zitashiriki Championship zimeshakuwa wazi.

    Tumeona namna ilivyokuwa kwenye ushindani wa kiatu cha ufungaji bora ulivyoibuka ghafla kati ya Fiston Mayele wa Yanga na Saido Ntibanzokiza wa Simba.

    Wote wamefunga mabao 17 kibindoni na kamati inasubiri ikae kikao iamue nani atakuwa mfungaji bora.

    Kutoka ligi ya Championship tayari timu za JKT Tanzania na Kitayosce zimefanikiwa kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2023/24.

    Kinachosuiriwa kwa sasa ni kutangazwa kwa ufunguzi wa dirisha la usajili na baadaye ratiba ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2023/24 ambao kwa kawaida hufunguliwa mwezi Agosti mwaka huu.

    Kimsingi tunaendelea kuwapongeza Yanga kwa kufanya kazi kubwa kiasi cha kuandika rekodi mbalimbali msimu huu kwenye michuano ya ndani na kule kimataifa, ikiwemo rekodi yao ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

    Kwa Ruvu Shooting na Polisi Tanzania tunaamini changamoto walizokutana nazo msimu huu zitakuwa chanzo cha elimu ya kujipanga upya kuelekea msimu ujao ili wapambanie nafasi ya kurejea Ligi Kuu.

    Kuelekea mwanzo mwa msimu mpya wa 2023/24 bila shaka kunaweza kutokea mabadiliko kidogo kwenye ratiba hasa kutokana na kuwepo kwa mabadiliko kadhaa ya tarehe rasmi ya kumaliza msimu huu.

    Hali hii pia kwa kiasi fulani ni wazi huenda ikaathiri ratiba ya maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’ kwa timu nyingi kwa kuwa kulinganisha na makadirio, kiasi timu zitakuwa na kipindi kifupi cha maandalizi ya msimu mpya.

    Katika hali kama hii huu ni muda kwa viongozi wakuu wa kiutendaji kwenye timu kuhakikisha wanaanza mipango ya maandalizi mapema ili kujiweka salama na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na kukosa muda wa maandalizi na kupelekea kuwa na matokeo mabaya uwanjani.

    Ipo mifano mingi ya timu ambazo zilikuwa na maandalizi ya kuungaunga ya kabla ya msimu, kiasi kwamba ligi zilipoanza wakajikuta kwenye wakati mgumu watoto wa mjini wanasema ligi ikawapalia na kujikuta wakishuka daraja.

    Msingi wa mafanikio ya jambo lolote ni maandalizi bora hivyo kwa timu zetu hili ni jambo la msingi sana kulifanyia kazi hususani kwa wale wageni wa ligi.

    Mwisho kila mmoja akumbuke kuwa waswahili walisema utavuna ulichopanda na muda ni hakimu asiye na huruma hivyo kila mtu apambane katika maandalizi bora ya kabla ya msimu kwa ajili ya matokeo bora mwishoni mwa msimu.

    Previous articleYANGA WASEPA NA UBINGWA WAO WA LIGI KUU BARA
    Next articleMATAJIRI WA MAFUTA WAMPIGIA SIMU MAYELE, KIBABE SANA