MAAJABU YA SOKA, MZUNGUKO WA 29 UMEACHA MENGI

    HUWEZI kuzuia mvua kunyesha kwa namna yoyote ile wakasema acha inyeshe tuone panapovuja. Soka lina maajabu yake na mzunguko wa 29 ulikuwa noma kinomanoma.

    Kwenye Ligi Kuu Bara wakati wa lala salama rekodi mpya zimeandikwa kwa timu kupata matokeo ambayo yameacha mshtuko huku wachezaji wakiweka rekodi zao.

    Hapa tunakuletea namna kazi ilivyokuwa mzunguko wa pili Juni 6,2023 namna hii:-

    Dakika 90

    Mabao matatu yalifungwa dakika ya 90 kwenye mechi tofauti na mastaa tofauti kwenye kutimiza majukumu yao.

    Ni Yanga walipata bao Uwanja wa Sokoine kupitia kwa Bernard Morrison dhidi ya Mbeya City, Azam FC walifunga bao moja kupitia kwa Prince Dube na Meddie Kagere wa Singida Big Stars aliwatungua Ruvu Shooting, Uwanja wa Liti.

    Mabao 27

    Viwanja 8 vilikusanya jumla ya mabao 27 ambayo yaliokotwa kwenye nyavu baada ya dakika 90 huku ubao wa Azam Complex ukisoma Simba 6-1 Polisi Tanzania ukikomba mabao mengi ambayo ni 7.

    Mchezo wa pili Uwanja wa Sokoine uliposoma Mbeya City 3-3 Yanga unafuata kukusanya mabao mengi ambayo ni saba.

    Kwenye viwanja nane ambavyo vilikuwa na msako wa pointi tatu ni Uwanja wa Sokoine pekee ulishuhudia timu zikigawana pointi mojamoja kati ya Mbeya City na Yanga huku viwanja saba ikiwa ni mwendo wa ushindi.

    Ndani ya 15 washatupia

    Mastaa watatu ndani ya dakika 15 walikuwa wametupia kwa wapinzani wao kwenye mzunguko wa pili.

    Ngoma ilifunguliwa na George Sangija wa Mbeya City aliyefanya yake dakika ya pili dhidi ya Yanga, Yacouba Songne wa Ihefu Uwanja wa Highland Estate alitupia dakika ya 14 dhidi ya Geita Gold.

    Saido Ntibanzokiza alifanya kazi yake dakika ya 15 dhidi ya Polisi Tanzania, Uwanja wa Azam Complex.

    Johora kaibuka

    Erick Johora kipa namba nne wa Yanga ameibuka kwa mara ya kwanza mchezo dhidi ya Mbeya City.

    Kwenye mchezo huo nyota huyo kashuhudia Kamba tatu zikizama kwenye nyavu zake, kipindi cha kwanza alitunguliwa mabao mawili na kipindi cha pili alitunguliwa bao moja.

    Kadi nyekundu

    Mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine ulishuhudia kadi nyekundu mbili nyekundu ikiwa ni kwa mchezaji mmoja wa Mbeya City ambaye ni Hassan Nassoro na Jesus Moloko wa Yanga.

    Tatu Malongo aliwaoyesha mastaa hao kadi nyekundu dakika ya 87 kwa kile walichoonekana kuonyeshana ubabe uwanjani.

    Kadi ya kwanza nyekundu kwa mabingwa Yanga nyekundu anaonyeshwa Moloko.

    Asante Polisi Tanzania

    Polisi Tanzania ni dakika zake 90 chungu ndani ya ligi wakipewa mkono wa asante jumlajumla ndani ya msimu wa 2022/23.

    Msimu ujao wa 2023/24 watakuwa ndani ya Championship baada ya kushuka daraja. Timu hiyo baada ya kucheza mechi 29 ina pointi 25 ina mchezo mmoja dhidi ya Azam FC wakufungia msimu.

    Inaungana na Ruvu Shooting yenye pointi 20 kibindoni zote zikiwa zimecheza mechi 29.

    Kujifunga

    Abdalah Mfuko wa Kagera Sugar, Uwanja wa Manungu kwenye jitihada za kuokoa hatari dakika ya 66 alijifunga akiwa ndani ya 18.

    Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Manungu ulisoma Mtibwa Sugar 3-0 Kagera Sugar na pointi tatu zikabaki Manungu.

    Nne zinapambana

    Timu nne kwa sasa zinapambana kujinasua kwenye mstari wa kucheza play off kubaki ndani ya ligi ama kushuka.

    KMC iliyo nafasi ya 14 na pointi 29, Mbeya City iliyo nafasi ya 13 ina pointi 31, Mtibwa Sugar nafasi ya 12 ina pointi 32 na Coastal Union iliyo nafasi ya 11 pointi 33.

    Imeandikwa na Dizo Click imetoka gazeti la Spoti Xtra.

     

    Previous articleVIGONGO VYA LIGI KUU BARA LEO HIVI HAPA
    Next articleSIMBA: NTIBANZOKIZA ATAKUWA MFUNGAJI BORA