HESABU za kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa zimeshafungwa kwa baadhi ya timu kutokana na kuvuna kile ambacho wamekipanda,
Yanga ni mabingwa wa ligi na wametinga hatua ya fainali ya Azam Sports Federation.
Ni dhidi ya Singida Big Stars walipenya kwenye nusu fainali na sasa watakwenda kumenyana na Azam FC, Mkwakwani Tanga.
Ruvu Shooting ya Pwani imekuwa ya kwanza kugotea mwisho ikiwa na mechi mbili mkononi baada ya kupambana kwa muda mrefu kusaka matokeo.
Ipo wazi kwamba miongoni mwa timu ambazo zilikuwa zinaleta ushindani ndani ya ligi huwezi kuiacha Ruvu Shooting ambayo ilikuwa na sera ya mpapaso.
Malengo yamekuwa magumu kutimizwa kwao msimu huu kutokana na sababu ambazo wao wanazitambua hivyo hizi ni lazima ziwe ni somo kwa wengine.
Ikumbukwe kwamba tangu mwanzo wa msimu Ruvu Shooting haikuanza vizuri hili lilitokana na aina ya usajili ambao walifanya pamoja na wachezaji wao wengine kuelekea kwenye masomo.
Kwa kilichotokea kwa Ruvu Shooting kinaweza kuwakuta wengine hata wale ambao wamepanda ligi kwa msimu ujao watakuwa na kazi ya kufanya kuboresha benchi la ufundi na aina ya wachezaji kwenye timu yao.
JKT Tanzania wanatambua ushindani uliopo kwenye ligi kwa kuwa walikuja kisha wakashuka na sasa wanarejea kwa mara nyingine tena.
Jambo la msingi ni kila timu kufanya maandalizi mazuri kwa msimu mpya ambao utakuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kupambana kusaka matokeo mazuri.
Ipo wazi kuwa ligi imekuwa na ushindani mkubwa na kila mchezaji anapenda kuona matokeo mazuri yakipatikana lakini hayatokei ghafla ni lazima kuwe na mpango kazi mzuri.