Home Sports YAJUE MAJEMBE YA KAZI NDANI YA SIMBA

YAJUE MAJEMBE YA KAZI NDANI YA SIMBA

MAJEMBE saba yanayovuja jasho la haki ndani ya kikosi cha Simba yamewapa kicheko Simba wakiamini kuwa hawajabahatisha kupenya kwenye orodha ya kuwania tuzo bali ubora umewabeba.

Ipo wazi kwamba Yanga ni mabingwa wa msimu wa 2022/23 huku Simba ikigotea nafasi ya pili.

Pia Yanga Mei 28 2023 inakwenda kucheza mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho na Simba wakiwa ni mashuhuda wa tukio hilo la kihistoria.

Katika orodha ya kuwania tuzo ndani ya ligi msimu wa 2022/23 tayari Kamati ya Tuzo Tanzania iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) imetaja mastaa waliopenya kuwania tuzo zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni huku Simba ikitoa mastaa saba.

Ni kwenye kipengele cha mchezaji bora ni nyota wawili wamepenya ambao ni Mzamiru Yassin na Saido Ntibanzokiza wote ni viungo.

Aishi Manula maarufu kama Air Manula kipa namba moja wa timu hiyo amepenya kwenye kuwania tuzo ya kipa bora akipambana na Djigui Diarra wa Yanga na Benedict Haule wa Singida Big Stars.

Watatu wamepenya kwenye tuzo ya beki bora ambao ni Shomari Kapombe, Henock Inonga na Mohamed Hussein sawa na watatu waliopenya kuwania tuzo ya kiungo bora ikiwa ni Clatous Chama, Mzamiru na Sadio.

Wakati wachezaji wao wakipenya na jina la kocha Roberto Oliveira nalo limetajwa kwenye kipengele cha kuwania tuzo ya kocha bora msimu wa 2022/23.

 Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa hilo ni jambo kubwa na linadhihirisha ubora walionao.

“Wachezaji wa Simba kutajwa kwenye orodha ya kuwania tuzo ni jambo linamaanisha kuwa kikosi kina wachezaji bora na wengi wametajwa kuwania tuzo hivyo mambo mazuri yanakuja,”.

Previous articleSERIKALI YAENDELEZA NEEMA KWA YANGA KIMATAIFA
Next articleKOCHA WA WAARABU AIPA YANGA KOMBE