MWENDELEZO mwingine wa ile burudani kwa kila timu kusaka pointi tatu baada ya safari kuwa ndefu kwenye mzunguko wa kwanza huku vinara wakiwa ni Yanga.
Kwa sasa ngoma ipo mzunguko wa pili kila timu zikipambana kusaka ushindi uwanjani.
Ni Mei yule Ng’ombe aliyekuwa anakatwa vipande vidogovidogo kama anakaribia kufikia kwenye mkia ila upepo unaweza kubadilika na mkia kuwa mkubwa kuliko Ng’ombe kutokana na matokeo ndani ya dakika 90.
Hapa tunakuletea kazi ngumu ndani ya Mei namna hii:-
Ngoma nzito wanapokutana hawa jamaa ndani ya dakika 90 unapigwa mpira mkubwa na jasho linavuja kinonoma itapigwa Mei 3,2023.
Katika mzunguko wa kwanza mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa Novemba 16,2022 ubao ulisoma Simba 1-0 Namungo, wanakutana kwa mara nyingine kukamilisha ngwe ya pili ugenini.
Namungo iliyo nafasi ya sita na pointi 35 hawana jambo dogo wanasaka pointi tatu kulipa kisasi huku Simba wakiwa na hesabu za kuendeleza rekodi ya ushindi ili waongeze pointi kwa kuwa wanazo 63 nafasi ya pili.
Singida Big Stars v Yanga
Kisasi kingine Mei 4,2023 kinatarajiwa kuwa Uwanja wa Liti baada ya Singida Big Stars kuwa timu ya kwanza kutunguliwa hat trick na Fiston Mayele, Uwanja wa Mkapa.
Kwenye mchezo huo ubao ulisoma Yanga 4-1 Singida Big Stars huku bao la kufuta machozi kwa Singida likifungwa na Meddie Kagere.
Kagere sio mnyonge ametupia mabao 7 kibindoni ndani ya Singida Big Stars iliyo nafasi ya 4 na pointi 51 huku Yanga wakiwa ni vinara na pointi zao ni 68 nafasi ya kwanza.
KMC v Singida Big Stars
Jamhuri Kihwelo, ‘Julio’kete yake ya kwanza baada ya kubeba mikoba ya Hitimana Thiery ambaye alifungashiwa virago aliambulia kichapo kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Jamhuri Dodoma ukisoma Dodoma Jiji 1-0 KMC.
Ngoma ilikuwa Aprili 22 na kete yake ya pili ni dhidi ya Singida Big Stars mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru ni Mei 12.
Ipo baada ya kucheza mechi 27 ipo nafasi ya 14 KMC na pointi zake ni 26 itakutana na Singida Big Stars yenye pointi 51 baada ya kucheza mechi 26.
Geita Gold v Mbeya City
Dhahabu zimetoka kutibuliwa na Wajelajela, Tanzania Prisons baada ya kushuhudia ubao wa Uwanja wa Nyakumbu ukisoma Geita Gold 1-3 Tanzania Prisons.
Kibarua kingine tena palepale Nyankumbu ni dhidi ya Mbeya City kutoka pale Mbeya ngoma itakuwa nzito kwani Mbeya City nayo imetoka kulipa kodi kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa Kaitaba ukisoma Kagera Sugar 1-0 Mbeya City.
Mbeya City nafasi yao ni 13 wana pointi 27 mikononi mwa Geita Gold wenye pointi 37 nafasi ya tano itapigwa Mei 13.
Azam FC v Namungo
Walipowafuata Uwanja wa Majaliwa yule Edward Manyama aliongoza kikosi cha Azam FC kupakua minyama ilikuwa dakika ya 28 na ubao ukasoma Namungo 0-1 Azam FC.
Inapigwa Uwanja wa Azam Complex kwa kila timu kusaka pointi tatu muhimu ni Mei 13.
Coastal Union v Ihefu
Bora ukutane na Yanga ile inayopeta kimataifa kwa wakati huu ila usiombe kukutana na Coastal Union ikiwa na jambo lake wanakuwa na balaa zito pale Uwanja wa Mkwakwani,Tanga.
Ni Ihefu wanatakuwa mikononi mwa Coastal Union iliyo nafasi ya 11 na pointi 30 kibindoni.Ngoma itakuwa Mei 14.
Kagera Sugar v Prisons
Miamba hii miwili inatarajiwa kukutana pale Uwanja wa Kaitaba Mei 14yalipo machinjio ya Kagera Sugar ilipowatuliza ndugu zao Mbeya City.
Ukicheki msimamo Kagera Sugar ipo nafasi ya 7 na pointi 35, Prisons imejichimbia nafasi ya 9 pointi 31.
Polisi Tanzania v Mtibwa Sugar
Katikati ya mwezi yaani kama ulikuwa unakula Ng’ombe mzima taratibu utakuwa unakaribia mkia au labda mkia uwe mkubwa kuliko Ng’ombe hapo itakuwa balaa.
Polisi Tanzania wenye pointi 22 watawakaribisha Mtibwa Sugar wenye pointi 29 ni Mei 15.