KIMATAIFA, MWENDO WA KUSAKA REKODI

    MCHEZA kwao hutunzwa ipo wazi lakini hata ugenini pia kuna uwezekano wa kucheza na kutunzwa ikiwa wawakilishi wa Tanzania kimataifa Simba na Yanga wakitumia makosaya wapinzani wao kwa umakini.

    Simba ina kibarua cha kutupa kete ya mwisho hatua ya makundi usiku wa kuamkia Aprili Mosi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca na Yanga wao dhidi ya TP Mazembe Aprili 2.

    Ngoma ni nzito kwa wote hapa tunakuletea namna kazi ilivyo kwa wawakilishi hao namna hii:-

    Ugenini ngoma nzito

    Kwenye mechi ambazo wamecheza ugenini Yanga imekuwa ni ngoma nzito kusepa na pointi tatu mazima.

    Mchezo wa kwanza walipoteza dhidi ya US Monastir kisha wakaambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Real Bamako.

    Katika mchezo huo licha ya kuanza kufunga mapema ngoma ilipinduliwa jioni na kuwafanya wagawane pointi mojamoja.

    Ndani ya dakika 180 katika mechi za ugenini Yanga imesepa na pointi moja na kuyeyusha pointi tano kwenye msako wa pointi sita ugenini.

    Simba wao mchezo wao wa kwanza ugenini walionja joto ya jiwe kwa kupoteza pointi tatu dhidi ya Horoya na ule wa pili walisepa na pointi tatu dhidi ya Vipers.

    Kwenye mechi tatu ambazo Simba imecheza ugenini katika msako wa pointi sita imesepa na pointi tatu ikiyeyusha pointi tatu.

    Ushambuliaji tatizo

    Kwenye mechi za ugenini hatua za makundi katika Kombe la Shirikisho Yanga rekodi zinaonyesha ina shida kwenye ushambuliaji kwa kuwa ni bao moja pekee safu hiyo imetupia.

    Ni Fiston Mayele alitupia kwenye mchezo dhidi ya Real Bamako nchini Mali.

    Simba ni bao moja pekee pia imefunga ilikuwa dhidi ya Vipers mtupiaji akiwa ni Henock Inonga dakika ya 19 akitumia pasi ya Moses Phiri.

    Ukuta kweye kazi ngumu

    Kwa upande wa ulinzi ukuta wa timu zote una kazi ngumu kutokana na kukutana na timu zenye kasi kwenye kusaka matokeo nyumbani.

    Yanga inakutana na TP Mazembe ambao wanahitaji kulipa kisasi cha kunyooshwa mabao 3-1 walipocheza Uwanja wa Mkapa.

    TP Mazembe 3-1 Real Bamako ni mchezo ambao walikuwa nyumbani Februari 12  na walipiga jumla ya mashuti 17 huku nane yakilenga lango ikiwa inamaanisha kuwa ni hatari wakiwa nyumbani kwenye kushambulia.

    Simba inatambua muziki mzito inakutana nao dhidi ya Raja Casablanca ambao ni vinara wa kundi na wakiwa nyumbani wanachapa tu.

    Februari 10 wakiwa Uwanja wa Mohamed V ulisoma Raja Casablanca 5-0 Vipers huku wakipiga jumla ya mashuti 17 langoni kwa wapinzani wao na ni mashuti 8 yalilenga lango.

    Licha ya kuwa wameshatinga hatua ya robo fainali wakiwa nyumbani hawana jambo dogo hivyo safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na Henock Inonga ina kazi kubwa kuwazuia hawa vinara.

    Rekodi bora

    Timu zote zina kazi ya kusaka rekodi bora ugenini kwenye mechi za kimataifa ambazo ni za mwisho hatua ya makundi.

    Yanga imetinga hatua ya robo fainali ikisepa na pointi tatu inauhakika wa kumaliza nafasi ya kwanza na kufunga kwa rekodi bora ugenini na kufanikiwa kuichapa TP Mazembe nje ndani.

    Simba mfupa mgumu dhidi ya Raja Casablanca ambayo haijapoteza ikiwa itashinda ugenini itaandika rekodi bora ya kuwatungua vigogo hao nyumbani kwenye mchezo wa mwisho katika makundi.

    Matokeo ya Simba kundi C

    Horoya 1-0 Simba

    Simba 0-3 Raja

    Vipers 0-1 Simba

    Simba 1-0 Vipers

    Simba 7-0 Horoya

    Matokeo ya Yanga kundi D

    Monastri 2-0 Yanga

    Yanga 3-1 Mazembe

    Bamako 1-1 Yanga

    Yanga 2-0 Bamako

    Yanga 2-0 Monastir

    Previous articleSIMBA KUIVAA RAJA CASABLANCA LEO
    Next articleHUYU HAPA KUPEWA MIKOBA YA ZIMBWE JR SIMBA