Home Sports HIVI NDIVYO NGOMA ILIVYOPIGWA MPAKA ROBO FAINALI

HIVI NDIVYO NGOMA ILIVYOPIGWA MPAKA ROBO FAINALI

NGOMA ilipigwa na mwisho wa siku timu nane zimetinga hatua ya robo fainali Kombe la Azam Sports Federation.

Hapa  tunakuletea namna kazi ilivyokuwa kwa wapambanaji hao kusaka ushindi namna hii:-

Simba 4-0 African Sports, Uwanja wa Uhuru

Ilikuwa Machi 2,2023 ambapo mabao ya Simba yalifungwa na Jean Baleke dakika ya 36,Kennedy Juma dakika ya 47, Mohamed Mussa dakika ya 69 na Jimsony Mwinuke dakika ya 90.

Katika mchezo huu Moses Phiri aliweka rekodi ya kutoa pasi mbili za mabao ilikuwa dakika ya 47 na 90 huku nyota watatu ambao ni Peter Banda, Mwinuke na Mussa walikuwa super sub.

Mwinuke na Mussa hawa walifunga wakitokea benchi huku Banda yeye akitoa pasi moja ya bao

Yanga 4-1 Tanzania Prisons

Moja ya mchezo bora uliokuwa na ushindani mkubwa huu unaingia kwenye orodha kutokana na kasi ya kila timu kusaka ushindi.

Dakika 45 hakuna timu iliyoona lango la mpinzani na mabao yote matano yalifungwa kipindi cha pili cha mchezo huo.

Ilikuwa ni Machi 3. Mabao ya Yanga yalifungwa na Bakari Mwamnyeto dakika ya 52,Clement Mzize alitupia mawili dakika ya 70 na 88 na moja mali ya Aziz KI ambaye alipachika bao dakika ya 84 kwa mkwaju wa penalti.

Ni Jumanne Elifadhil huyu alipachika bao kwa upande wa Tanzania Prisons ambalo lilikuwa la kuvutia machozi.

Singida Big Stars 1-0 JKT Tanzania

Matumaini ya wengi yakiwa yameanza kuyeyuka kwa mashabiki wa Singida Big Stars kutinga hatua ya robo fainali ndani ya dakika 90 mkombozi akatokea ghafla.

Ni Biemes Carmo huyu alitupia bao jioni dakika ya 90 na kuwanyanyua mashabiki kwa shangwe na timu hiyo yenye maskani yake Singida kukata tiketi ya kutinga robo fainali.Ilikuwa ni Machi 3, Uwanja wa Liti.

Geita Gold 3-1 Green Warriors

Vijana wa Felix Minziro walionesha ubabe wao mbele ya wajeda, Green Warriors ambao walikuwa Uwanja wa Nyankumbu.

Inaungana na timu nyingine kwenye hatua ya robo fainali baada ya kupenya kwenye 16 bora ilikuwa Machi 3.

Ihefu 2-0 Pan African

Hawana jambo dogo Ihefu wakiwa kwenye ngome yao pale Highland Estate walipenya hatua ya robo fainai kwa kuitungua Pan African.

Ni Andrew Simchimba alipachika mabao yote mawili na kuizamisha meli ya Pan ilikuwa dakika ya 23 na 47 ilikuwa Machi 4.

Azam 2-0 Mapinduzi

Azam FC imetinga hatua ya robo fainali kwa ushindi dhidi ya Mapinduzi Uwanja wa Azam Complex.

Mtibwa Sugar 1-0 KMC

Msumari mmoja wa David Kameta, ‘Duchu’ dakika ya 45 kwa mkwaju wa penalti uliwafungashia virago KMC kwenye mashindano haya ilikuwa ni Machi 4,Uwanja wa Manungu.

Kagera Sugar 0-1 Mbeya City

Wakiwa nyumbani Kagera Sugar pale Uwanja wa Kaitaba mambo yalikuwa magumu kwao baada ya kutunguliwa na Richardson Ng’ondya

Nyekundu zilitembea

Ibraham Abraham beki wa Tanzania Prisons kwenye hatua ya 16 bora anaingia kwenye orodha ya nyota ambao walionyeshwa kadi nyekundu.

Huyu alionyeshwa kadi mbili za njano na kupelekea kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 45 na mwamuzi wa kati. Kadi ya kwanza ya njano alionyeshwa dakika ya 33 alimchezea faulo Jesus Moloko na ile ya pili dakika ya 44 alimchezea faulo Tuisila Kisinda.

Chalamanda

Ramadhan Chalamanda nyota wa Kagera Sugar ambaye ni kipa huyu alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mchezo dhidi ya Mbeya City.

Previous articleSIMBA HII FA’ MASIHARA NINI, BAMAKO WANACHAKAA
Next articleYANGA KAMILI KUIVAA BAMAKO, AZIZ KI, MAYELE NDANI