VITA YA MABINGWA NA WAJELAJELA

  INGEKUWA ni mchezo wa Ligi Kuu Bara tungesema ni tatu zinasakwa ndani ya tatu kwa wababe wawili ambao watavuja jasho ndani ya dakika 90.

  Bahati nzuri ni hatua ya 16 bora Kombe la Azam Sports Federation ambapo yule atakayetunguliwa inakuwa ni kwaheri ya kuonana wakati ujao.

  Ni vita ya mabingwa watetezi Yanga chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi raia wa Tunisia ambaye alikoingoza kikosi hicho kutwaa ubingwa dhidi ya Coastal Union ya pale Tanga.

  Ngoma inatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Azam Compelex saa 1:00 na kazi ya Yanga itakuwa ni dhidi ya Tanzania Prisons ambapo hawa ni wajelajela wenye maskani yao pale Mbeya.

  Huyu hapa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe akizungumzia kuhusu mchezo huo:-

  “Yanga tuna malengo ambayo tumejiwekea na tunapambana nayo kuhakikisha kwamba yanatimia na ili yatimie ni lazima kila mchezo tuuchukue kwa hali ya umakini mkubwa

  “Kwenye kombe la Shirikisho sisi ni mabingwa watetezi hilo lipo wazi na tuna mchezo wetu wa hatua ya 16 bora dhidi ya Tanzania Prisons tunawaheshimu wapinzani wetu kwa kuwa ni timu bora lakini lazima nasi tufanye kweli.

  “Ukiwa ni bingwa mtetezi maana yake huwezi kukubali kuliacha taji hilo ni taji muhimu na tunalitaka hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi.

  Unadhani itakuwa rahisi kushinda dhidi ya Prisons?

  “Ni moja ya timu nzuri ambazo tunakutana nazo na tuna amini kwamba kwa muda ambao tunao pamoja maandalizi kwa benchi la ufundi hilo litatufanya tupate matokeo mazuri.

  “Kila mmoja anahitaji kuona matokeo yanakuwa mazuri kikubwa mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kuongeza ule mshikamano ambao upo.

  Mataji mangapi mnataka kubeba msimu huu?
  “Tumeanza na Ngao ya Jamii hili lipo kwenye kabati letu na kwa sasa tupo kwenye kulisaka hili la Shirikisho ambalo lina umuhimu mkubwa.

  “Kutwaa taji hili kutafanya tuongeze ile idadi ya mataji ambayo tunahitaji kuyabeba ambayo ni matatu tulifanya hivyo msimu uliopita hili ambalo tunatetea pamoja na ligi ambalo hili tunaongoza kwenye msimamo tukiwa tumewaacha wapinzani wetu kwa pointi ambazo ninadhani ni 8 kwa sasa bado tupo sehemu nzuri.

  Kipi mashabiki watarajie?

  “Tunapeleka burudani pale Chamazi kwa kuwa mechi zetu za sasa tutatumia Uwanja wa Azam Complex ipo wazi Uwanja wa Mkapa unafanyiwa marekebisho hivyo tunakwenda Chamazi.

  “Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuipata ile burudan ambayo walikuwa wameikosa kwa muda na inawezekana wakaona kitu kizuri kutoka kwa wachezaji.

  “Huu ni mchezo muhimu kwetu tupo tayari na tunakwenda kufanya kazi kubwa kusaka ushindi ukizingatia kwamba ni hatua ya mtoano ukifanya kosa unaondolewa moja kwa moja,”.

  Jumanne Elifadhil nyota wa Tanzania Prisons ameweka wazi kuwa wanatambua mchezo huo ni muhimu kwao lakini hesabu kubwa wanazofikiria ni kufanya vizuri kwenye ligi.

  “Tunatambua kwamba mchezo wetu dhidi ya Yanga ni muhimu tutapambana kufanya vizuri huku hesabu zetu zikiwa kwenye nafasi yetu kwenye ligi,”.

  Previous articleMAJANGA SIMBA KIUNGO WA KAZI AVURUGA MIPANGO
  Next articleFEISAL ARUDISHWA YANGA