KILICHOWAMALIZA SIMBA, KILIWALIZA YANGA KIMATAIFA

KWENYE anga za kimataifa kilichowaua Simba ugenini kiliwamaliza Yanga pia ugenini kutokana aina ya mabao ya mapigo huru yaliyowapa tabu wawakilishi wa kimataifa.

Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika walianza kuonja joto ya jiwe kwenye msako wa pointi tatu dhidi ya Horoya ya Guinea ilikuwa ni Februari 11.

Wakati ubao wa Uwanja wa General Lansana Conte ukisoma Horoya 1-0 Simba bao la ushindi lilipachikwa na Pape N’Diaye dakika ya 18 akiunganisha krosi ya kona iliyopigwa kwenye mchezo huo.

Jitihada za Simba kusaka angalau pointi moja ziligota mwisho na mpaka mchezo unakamilika walipoteza kwa bao hilo pekee wakiwa ugenini.

Simba ipo kundi C ikiwa haijakusanya pointi sawa na Vipers ya Uganda huku Horoya ikiwa na pointi tatu nafasi ya pili vinara ni Raja Casablanca ya Morocco ambao watakutana nao Februari 18, Uwanja wa Mkapa.

Watani zao wa jadi Yanga, Februari 12 hawa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi ubao wa Uwanja wa Olympique de Rades ulisoma US Monastir 2-0 Yanga.

Mabao yote mawili yalifungwa kutokana na mapigo huru ambapo lile la awali lilifungwa na Mohamed Saghroui dakika ya 10 ilitokana na pigo la faulo na lile la pili lilifungwa na Boubacar Traore dakika ya 15 kwa pigo la kona huku mpigaji akiwa ni Heychecut Chikhaoui.