Home International MASHABIKI MOROCCO,PAMBO LA WORLD CUP

MASHABIKI MOROCCO,PAMBO LA WORLD CUP

Saleh Ally, Rabat

UTAMADUNI wa ushangiliaji katika soka uko tofauti karibu kila ukanda, na unaweza kutofautiana kwa bara moja zaidi ya sehemu nne au tano.

Mfano angalia ushangiliaji wa soka la Tanzania, una tofauti kubwa sana na ushangiliaji wa soka la Kaskazini mwa Afrika katika nchi kama Misri au Morocco.

Sifa kubwa ya ushangiliaji hapa Morocco wanayo Raja Casablanca ambao wanaaminika ndio bora zaidi katika nyanja hiyo ya ushangiliaji.

Namna wanavyojipanga, namna wanavyoupamba uwanja na kadhalika. Hakika ni burudani inayoongeza burudani nyingine ndani ya mchezo wa soka na hii ndio ni sehemu ya inayoongeza thamani na ushawishi wa mashabiki kwenda uwanjani.

Mashabiki wanajitokeza kwa wingi sana hata kama timu si ya Morocco, mfano tuliona mechi ya kwanza wakati Ahly wakicheza na Aucland City kwenye mji wa Tangier, mashabiki walikuwa wengi sana.

Hii maana yake hata baada ya wenyeji Wydad kutolewa, maana yake bado kuna nafasi ya mashabiki kwenda kwa wingi kuishuhudia michuano hiyo ambayo imefanyika Afrika, hii mara ya tatu na mara zote hapa Morocco.

Yes mashabiki watakwenda, lakini lazima tukubali kuwa burudani ya mashabiki wa Wydad itakosekana. Burudani ambayo ina aina yake pekee ya uendeshwaji au aina yake.

Mashabiki hao huingia uwanjani takribani saa tatu hivi kabla ya mechi na baada ya hapo, huanza kujipanga kwa mfumo wao sahihi.

Kunakuwa na viongozi kama saba hivi ambao hauwezi kuamini, wanasikilizwa zaidi ya kamanda wa jeshi. Maana kila wanachosema, basi kinatekelezwa mara moja.

Mpangilio wa ukaaji unaanza na kila mmoja baada ya kupangwa, mashabiki hao mfano kwenye mechi iliyopita walikuwa kama 10,000 hivi wanapewa vipeperushi maalum ambavyo wao wanajua namna ya kuvitumia wakati ukifika.

Baada ya hapo wanaanza kupasha mwili kwa kushangilia kama vile wanaseti mitambo kuhakikisha wakati wa mechi wanakuwa tayari kwa ajili ya kazi hiyo.

Taratibu wanakwenda wanaongeza nguvu na unapofikia wakati wa mechi wanakuwa tayari kwa kazi yao ambayo pia inakuwa katika mpangilio maalum.

Wanajua washangilie namna gani wakati inakwenda kupigwa faulo upande wao au upande wa wapinzani. Washangilieje wakati wanashambuliwa au wanashambulia na hata iweje baada ya kuwa wamefungwa bao.

Kwa kifupi ni muda wote wa dakika 90 watashangilia lakini kwa mifumo tofauti ambayo yote itakuvutia na hakika sauti yao inaweza kufanya usisimke katika ile hali ya kuipata tofauti burudani ya mchezo wa soka.

Sasa burudani ya mashabiki wa Wydad ambao wanaonekana hawawafikii Raja Casablanca imewachanganya kabisa ambao si watu wa Morocco walipohudhuria mechi hiyo.

Asilimia kubwa ya wadau wa mpira wamekuwa wakijijadili na kuamini kama itafanyika katika nchi zao itaongeza utamu na thamani ya mpira wao.

Kama Morocco wakifanikiwa kushinda nafasi ya kuandaa michuano ya Kombe la Dunia 2026, maana yake moja ya tunu na burudani watakuwa ni mashabiki wake.

Bila shaka kama Morocco wataungana, kutakuwa hakuna tena ushabiki wa timu fulani na fulani na nilikuwa najiuliza watafanya pamoja au kila upande utapewa mechi maalum?

Maana timu za Casablanca ndio zina nguvu sana na ni wapinzani wakubwa sana. Watakubali kufanya kazi pamoja? Lakini hata kama wakipewa mechi kwa mechi ninaamini kazi inaweza ikafanyika. Hakika mashabiki hawa ni ua la soka la Morocco.

Kombe la Dunia limefanyika mara moja tu Afrika, mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na sasa ni miaka 13 imepita na kufikia 2026 itakuwa imefikia 16, bila shaka utakuwa ni wakati wa Morocco na wanastahili.

Previous articleJOB NA AZIZ KI WALIMALIZA KAZI MAPEMA
Next articleLIGI KUU TANZANIA BARA KUKIWASHA LEO