Home Sports KAKOLANYA ATAJWA AZAM FC

KAKOLANYA ATAJWA AZAM FC

IMEFAHAMIKA kuwa, Azam FC, imeanza mazungumzo ya kimyakimya kwa ajili ya kuipata saini ya kipa namba mbili wa Simba, Beno Kakolanya.

Kakolanya hivi sasa amekuwa hana nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Simba, huku mkataba wake ukitajwa kumalizika mwisho wa msimu huu.

Taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, zinasema kwamba, yapo mazungumzo ya siri yanayofanywa kati ya kipa huyo na mabosi wa Azam.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, uzoefu na ubora alionao Kakolanya, ndio umewashawishi Azam kumfuata kwa ajili ya kumsajili.

Aliongeza kuwa, kama mazungumzo hayo yakifikia hatua nzuri, basi Kakolanya atasaini mkataba wa kuichezea Azam.

“Tumepanga kukifanyia maboresho kikosi chetu katika usajili huu wa dirisha dogo.

“Tayari tupo katika mazungumzo na baadhi ya wachezaji, kati ya hao yupo Kakolanya ambaye tumeanza naye mazungumzo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kaimu Ofisa Habari wa Azam, Hasheem Ibwe, alizungumzia usajili kwa kusema kuwa: ” Tumepanga kufanya usajili mkubwa katika dirisha dogo wa kimyakimya, watu hawataamini.”

Azam FC inatajwa kuwa kwenye wakati wa kusaka kipa mwingine baada ya kipa namba moja wa kikosi hicho, Ali Ahmada raia wa Comoros kuonekana kutofiti eneo hilo.

Previous articleWAARABU WAMFUATA AZIZ KI YANGA SC
Next articleMIDO AS VITA AFUNGUKA KUTUA YANGA