Home International KOMBE LA DUNIA ROBO FAINALI ZA KIBABE

KOMBE LA DUNIA ROBO FAINALI ZA KIBABE

MECHI za hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Dunia zinatarajiwa kuanza kazi leo Ijumaa ambapo miamba wa soka Ulaya na Amerika Kusini inatarajia kupambana.

Mechi ya mapema zaidi leo Ijumaa inatarajiwa kuwa kati ya Croatia dhidi ya Brazil majira ya saa 12:00 jioni kwa Bongo halafu baadaye Uholanzi wakimenyana na Argentina saa 4:00 usiku Uwanja wa Lusail Iconic.

 Hapa kuna uchambuzi wa mechi hizi kama ifuatavyo;

UHOLANZI V ARGENTINA

Hii ni mechi ambayo imejaa ushindani mkubwa kwa siku ya leo na hii ni kutokana na upinzani uliopo baina yao.

Argentina na Uholanzi wanakutana kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka nane.

Miamba hii ina historia kubwa kwenye Kombe la Dunia ambapo imekutana mara tisa, mechi tano kati ya hizo ni za Kombe la Dunia.

Ni Waholanzi waliibuka kidedea mara nne na Argentina mara tatu huku wakitoka sare mechi mbili.

Mshindi wa hapa ataenda kukutana na mshindi kati ya Croatia na Brazil.

Argentina waliwafunga Uholanzi kwenye mechi ya fainali ya michuano hiyo kwa mabao 3-1 mwaka 1978 kwenye ardhi ya nyumbani. Na ile fainali ya pili wakaibanjua Ujerumani Magharibi kwa mabao 3-2 mwaka 1986.

Kitendo cha kukutana tena kwa timu hizi kwenye Kombe la Dunia ni ishara kwamba upinzani wao umekuwa mkubwa hali inayoongeza ushindani baina yao.

Uholanzi ilianza michuano ya mwaka huu kwa kutoa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Afrika, Senegal kabla ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Ecuador. Mechi iliyofuata wakamfunga mwenyeji Qatar kwa mabao 2-0.

Baada ya hapo wakatinga mtoano na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Marekani na kucheza mechi 19 bila kufungwa.

Kwa upande wao Argentina walianza michuano kwa kushtua kwani walichapwa mechi yao ya kwanza kwa mabo 2-1 na Saudi Arabia, mchezo wa pili walishinda mabao 2-0 dhidi ya Mexico kabla kuibanjua Poland 2-0. Katika hatua ya 16 Bora waliiondosha Australia kwa mabao 2-1.

HISTORIA YAO

Uholanzi walikuwa na timu bora ambazo zilishindwa kubeba taji licha ya kucheza fainali hizo mwaka 1974, 1978 na 2010.

Mara zote waliishia kuwa washindi wa pili huku wakitolewa hatua ya nusu fainali mara mbili mwaka 1998 na 2014.

Uholanzi iliibomoa Argentina mabao 4-0 walipokutana kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi mwaka 1974.

Wakatinga fainali ambayo walienda kulia kwa kufungwa na Ujerumani Magharibi.

Miaka minne baadaye,  Argentina ililipiza kisasi kwa Waholanzi kwenye ardhi ya nyumbani huko Buenos Aires kwa ushindi wa 3-1 katika muda wa ziada.

Waholanzi walipata ushindi mkubwa miaka 20 baadaye katika robo fainali mwaka 1998 nchini Ufaransa na kufungwa na Brazil katika nusu fainali.

Ya mwisho kukutana ilikuwa kwenye nusu fainali ya mwaka 2014 ambapo Argentina walishinda kwa penalti 4-2 kufuatia suluhu katika muda wa kawaida na ule wa ziada, Argentina waliwashinda Waholanzi katika mikwaju ya penalti na kutinga fainali kwa mara ya kwanza tangu 1990.

WACHEZAJI WA KUCHUNGWA

Nahodha wa Argentina, Lionel Messi ambaye hadi sasa ana mabao matatu ndiye mchezaji wa kuchungwa zaidi kwenye mchezo huu, kwenye mchezo dhidi ya Australia, alifunga bao lake la 94 katika mechi 169 za kimataifa.

Messi anaitaka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa michuano hii baada ya kuigaragaza rekodi kama hii ngazi ya klabu huyu ndiye mwenye ufunguo wa kuamua Argentina ifike hatua gani kwenye michuano hii.

Kwa upande wa Uholanzi, wao wana safu nzuri ya ulinzi chini ya Virgil van Dijk ambayo imeruhusu mabao mawili tu hadi sasa. Nyota ambao ni tegemeo zaidi ni Memphis Depay na Cody Gakpo ambao ndio wataongoza safu ya ushambuliaji.

Croatia  v      Brazil

Mchezo huu haupewi kipaumbele sana kama ilivyo kwa Argentina v Uholanzi labda kwa kuwa Brazil inaenda kukutana na timu inayobezwa ya Croatia.

Ukiangalia takwimu zao utaona kuwa Croatia sio timu ya kubezwa kwani walicheza fainali ya mwaka 2018 na wakafungwa na Ufaransa. Walianza mashindano ya mwaka huu kwa suluhu dhidi ya Morocco kisha wakashinda mbele ya Canada na wakatoa suluhu na Ubelgiji.

Kwenye hatua ya mtoano wamewaondosha Japan kwa penalti 3-1.

Kurejea kwa Neymar kwenye kikosi cha Brazil kunaifanya timu hiyo ipewe nafasi kubwa ya kupenya huku wakionyesha kiwango bora kwenye mtoano kwa kuwaondosha Korea Kusini kwa mabao 4-1. Mechi hii itapigwa Uwanja wa Education City mjini Al Rayyan.

Previous articleVIDEO:JEMBE:KIPA WA NAMUNGO KAWAFUNGISHA,MAKIPA WAGENI SIO WA AFYA
Next articleVIDEO:JEMBE AICHAMBUA SIMBA YA ZAMANI/REKODI HAIJAVUNJWA