Home International URENO YATEMBEZA DOZI IKITINGA ROBO FAINALI

URENO YATEMBEZA DOZI IKITINGA ROBO FAINALI

TIMU ya Taifa ya Ureno imetembeza dozi kwa wapinzani wao kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora Kombe la Dunia Qatar.

Bila ya uwepo wa Cristiano Ronaldo ambaye alianzia benchi na mbadala wake Goncalo Ramos kwenye mchezo wa kuwania kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Dunia mpira ulitembea.

Ushindi wa mabao 6-1 walioupata dhidi ya Uswisi unawapa tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali Kombe la Dunia Qatar,2022.

Ramos alifunga hat trick kwenye mchezo huo na kusepa na mpira wake ilikuwa dakika ya 17,51 na 67 na mabao mengine yalifungwa na Pepe dakika ya 33, Raphael Guerreiro dakika ya 55, Rafael Leao dakika ya 90 na lile la Uswisi lilifungwa na Akanji dakika ya 58.

Ulikuwa mchezo wenye ushindani na dunia imeshuhudia Ureno ikitinga hatua ya robo fainali tangu ilipofanya hivyo 2006

Ramos, ambaye alikuwa ni mbadala wa Ronaldo alikuwa na miaka mitano wakati Ronaldo anafunga bao lake la kwanza kwenye mashindano ya Kombe la Dunia na alitumia dakika 17 kufunga bao hilo.

Kocha Mkuu wa Ureno, Fernando Santos amesema kuwa hakuna tatizo kuhusu mchezaji  wao Ronaldo kwa kuwa ni mchezaji ambaye anajua majukumu yake.

“Nadhani suala la Ronaldo tayari tumeshatatua. Ninarudia mwenyewe kama ambavyo nilisema kwenye vikao vilivyopita, ni jambo ambalo limekwishwa na hakuna tatizo.

“Tunachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuangalia mechi zetu zijazo, kwenye histora yeye ni mchezaji mzuri ni miongoni mwa wale ambao wamefunga mabao mengi kumbuka kwamba ni nahodha pia tuna uhusiano mzuri naye,”.

Kocha Mkuu wa Uswisi, Murat Yakini amesema kuwa kufungwa ni maumivu ambayo hayazoeleki kwa kuwa walijipanga kupata ushindi kwenye mchezo huo.

“Kulikuwa na mabadiliko kwenye mfumo lakini hayakuwa makubwa.Tulifanya kiasi chake kwenye mpango wetu ambao haukufanikiwa kutupa majibu na tumeshindwa mchezo wetu ambapo wapinzani wetu walitawala mchezo

“Tunakubali kwamba wale wapinzani wetu walikuwa na haraka sana kwenye maamuzi na kufanya ulinzi mgumu ambacho ninaweza kusema mpango kazi wetu haukufanya kazi, ninawapongeza Ureno kwa ushindi yale makosa tunayachukua kuyafanyia kazi,”

Matokeo hayo yataifanya Ureno kumenyana na Morocco kutoka Afrika kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali, Jumamosi, Desemba 10.

Previous articleYANGA IMEWAPIGIA SIMU WASHAMBULIAJI WAWILI
Next articleKOCHA HISPANIA AKUBALI UWEZO WA BONO