Home Sports TIKETI 10,000 MASHABIKI WA YANGA KUPEWA KUWAONA WAARABU

TIKETI 10,000 MASHABIKI WA YANGA KUPEWA KUWAONA WAARABU

UONGOZI wa Yanga umetangaza kugawa bure tiketi 10,000 za mchezo wa Yanga dhidi ya Club Africain ya nchini Tunisia kwa mashabiki watakaochanja chanjo ya Uviko-19.

Yanga wanatarajiwa kukutana na Club Africain Novemba 2 katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

 CEO wa Yanga, Andre Mtine, amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa wanaendelea kutoa elimu juu ya magonjwa ya Uviko-19, watatoa chanjo kwa mashabiki 10,000 ambao watachanjwa, hivyo jambo hilo kwao wanafanya kama sehemu ya kuelimisha jamii.

“Ushirika wetu na UNICEF kuhusu Uviko-19 na virusi vya Ebola umeanza kazi rasmi ambapo tunatoa zawadi ya tiketi 10,000 kwa mashabiki ambao watachanja chanjo ya Uviko-19 kushuhudia mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tarehe 2 mwezi ujao,” amesema.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema:“Kila mmoja wetu anafahamu madhara ya Uviko-19, hivyo kupambana na Uviko-19 ni jukumu letu sote. Sisi kama Klabu tunatamani mitaa iwe salama.

“Hatuwezi kutoa burudani kama hatutoi elimu ya afya. Tumeandaa vitu mbalimbali, na utakutana na viongozi mbalimbali wa klabu yetu ambao watakuja kutoa hamasa. Mayele, Feisal na Aziz Ki pamoja na wachezaji wengine watakuwepo mitaani kutoa elimu hiyo na kuhamasisha” amesema Kamwe.

Previous articleSIMBA YAPIGA 5G, MTIBWA MAJANGA KADI NYEKUNDU ZAWAPONZA
Next articleAZAM FC KUIKABILI IHEFU