KWENYE JUMUIYA YA MADOLA TANZANIA IMEPATA MEDALI

TANZANIA imehitimisha ushiriki wake katika Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola  jijini Birmingham, Uingereza, ikiwa katika nafasi ya 28 baada ya mategemeo yake manne ya mwisho kushindwa kuambulia chochote.

Kwanza alianza bondia Yusuf Lucasi Changalawe kwa kupambana na  Sean Lazzerini wa Scotland katika nusu finali ya kwanza ya uzani wa 75kg-80kg (Light Heavyweight ) katika Ukumbi Namba 4 wa National Exhibition Centre (NEC) ambapo alishindwa kwa pointi.

Tegemeo la pili lilikuwa kwa bondia Kassim Selemani Mbundwike aliyepambana kishujaa na bondia Tiago Osorio Muxanga wa Msumbiji katika nusu finali ya pili ya uzani wa 67kg-71kg (Light Middle) katika Ukumbi huohuo, lakini naye akazidiwa pointi.

Hata hivyo, kwa mabondia Changalawe na Mbundwike kucheza hatua hiyo ya nusu fainali imemaanisha kwamba kila mmoja wao tayari ana medali ya shaba, kwani katika ndondi mabondia wote wanaofika hatua hiyo huwa moja kwa moja wanatunukiwa medali hiyo, hata kama watashindwa katika mchezo wao wa nusu fainali.

Karata nyingine mbili zilizosalia walikuwa nazo wanariadha Josephat Joshua Gisemo na mwenzie Faraja Lazaro Damasi ambao walikimbia bega kwa bega katika dimba moja katika fainali ya mbio za  mita 5,000 Uwanja wa Alexander, wakiwa miongoni mwa wanariadha 20 kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola waliowania medali za Dhahabu, Fedha na Shaba.

Pamoja na juhudi kubwa walizofanya lakini Watanzania hawa walimaliza katika nafasi za 15 na 16, huku Jacob Kiplimo wa Uganda akishika nafasi ya kwanza akifuatiwa na Wakenya N. Kimeli aliyebeba medali ya Fedha na J. Kiprop alyeondoka na medali ya Shaba.

Hivyo kimsimamo Tanzania inashika nafasi ya 28 katika nchi ambazo zimeambulia medali.  Takriban wanamichezo 5,054 wanashiriki katika michezo hiyo kutoka nchi 72 ambapo jumla ya michezo 20 huchezwa.

Jirani zetu Kenya ni wa 12 kimsimamo kwa kuwa na jumla ya medali 16 ikiwa ni 4 za dhahabu, 5 za Fedha na 7 za Shaba. Uganda ni ya 13 kwa kuwa na medali  tatu za Dhahabu na mbili za Shaba.

Bara la Afrika  linaongozwa kimsimamo na  Nigeria na Afrika ya Kusini  katika kupata medali nyingi ambapo Nigeria ni ya 6 kimsimamo kwa kupata jumla ya medali 16, ambapo 9 ni Dhahabu, 8 ni Fedha na 13  ni Shaba.