ISHU YA KAMBI YA YANGA MORO IPO HIVI

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa suala la kambi kwa maandalizi ya msimu wa 2022/23 lipo mikononi mwa benchi la ufundi.

Mpango wa awali wa Yanga kuweka kambi ilikuwa ni nchini Tunisia na imeelezwa kuwa mpango huo umewekwa kando kutokana na muda kutajwa kuwa mdogo.

Pia habari zinaeleza kuwa kwa sasa wanatarajia kwenda kuweka kambi pale ilipo milima ya Uluguru,Morogoro lakini haijawa wazi mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Thabit Kandoro,Mkurugenzi wa Mashindano Yanga amesema kuwa kocha ndiye mwenye maamuzi ya wapi kambi itakuwa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

“Suala la wapi Yanga inatakiwa kwenda kufanya kambi kwa maandalizi ya msimu ujao linabaki kuwa jukumu la benchi la ufundi na mwenye uamuzi wa wapi kambi inatakiwa kuwa ni kocha Nasreddine Nabi mwenyewe.

“Kama ataamua kwenda nje ya nchi timu itakwenda na kama anataka tubaki Dar au nje ya mkoa hata akisema Morogoro hatuna tatizo hatuna tabia ya kuiga watu fulani kwamba wapo fulani basi nasi tuende hapana,” amesema.

Yanga msimu ujao wanatetea mataji matatu ikiwa ni pamoja na Ngao ya Jamii,ligi na Kombe la Shirikisho.