TIMU ya vijana chini ya miaka 17 ya Azam FC imetwaa ubingwa wa ligi ya Vijana wa umri huo baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Karume.
Azam FC waliingia kwenye mchezo huo wakihitaji sare tu ili kuwa mabingwa baada ya kujikusanyia alama 25 katika michezo 9 iliyokuwa imeshafanyika.
Hivyo kwenye mchezo huo uliochezwa jana ambao ulikuwa ni wa 10 sare tu ingetosha kuwahakikishia ubingwa lakini vijana hao wa Mohamed Badru hawakutaka kubahatisha kwani walicheza kwa nguvu na maarifa makubwa na kuutawala mchezo.
Dakika ya tano tu ya mchezo, Abdulkareem Kiswanya akaipatia Azam FC bao la kwanza akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo kutoka upande wa kushoto wa Uwanja wa Karume.
Dakika ya 30 Azam FC wakapata penati iliyopigwa na Cyprian Kachwele lakini ikaokolewa na kipa wa Yanga ambaye alikuwa imara langoni kwa wakati huo.
Hadi mapumziko matokeo yalikuwa 1-0 kwa faida ya Azam FC. Kipindi cha pili Kachwele akarekebisha makosa yake ya kukosa penati na kufunga bao maridadi kwa mguu wa kushoto.
Bao hilo likatosha kuihakikishia Azam FC ushindi katika mchezo ambao Azam FC waliutawala kwa kiasi kikubwa.Hadi wanatawazwa kuwa mabingwa, Azam FC imebakiwa na michezo miwili mkononi, baada ya kucheza michezo 10, wakishinda 9 na kutoa sare mmoja.
Wamefunga mabao 30 na kufungwa manne tu.Na mshambuliaji wa Azam FC, Cyprian Kachwele, anaongoza mbio za ufungaji bora akiwa na mabao 14.