Home Sports KOCHA WA VIWANGO ATUA SIMBA, ASHAFIKA HATUA YA NUSU FAINALI KOMBE LA...

KOCHA WA VIWANGO ATUA SIMBA, ASHAFIKA HATUA YA NUSU FAINALI KOMBE LA AFRIKA

SIMBA msimu ujao itakuwa chini ya Kocha Mserbia, Zoran Manojlović, 59, ambaye anarekodi ya kufundisha klabu kubwa barani Afrika.

Mei 31, mwaka huu iliachana na kocha wao Pablo Franco baada ya kutoka kufungwa na Yanga bao 1-0 kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam na kuzima ndoto ya timu hiyo kubeba kombe hata moja.

Rekodi za kocha huyo zinaonyesha kuwa alifundisha klabu vigogo Afrika. Klabu ya kwanza kutaa Afrika kuinoa ilikuwa Primeiro de Agosto kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 akiwa hapo aliifikisha nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya hapo akaenda zake Wydad Athletic Club ya Morocco alidumu kwa msimu mmoja kuanzia mwaka 2019 hadi 2020 na msimu uliofuata akaenda zake Al Hilal ya Sudan.

Safari yake haikuishia hapo kwani Aprili mwaka 2021 alienda kukinoa kikosi cha CR Belouizdad cha nchini Algeria hakukaa sana Agosti 30, mwaka jana akatambulishwa kuwa kocha wa Al-Tai ya Saudi Arabia ambapo alidumu hadi Novemba 4 akatimuliwa kutokana na timu kuwa kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi.

Katika ufundishaji wake soka, Manojlović amefanikiwa kutwaa kombe moja la Ligi Kuu ya Algeria akiwa na CR Belouizdad.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka Simba, klabu hiyo tayari imemalizana na kocha Mserbia Manojlović ambaye alianza kazi ya kufundisha soka kule nchini Ureno na muda wowote kuanzia jana alitarajia kutangazwa.

Mtoa taarifa huyo alidai kuwa, kocha huyo ataanza kazi haraka na amepewa jukumu la kusuka upya kikosi kwa ajili ya michuano ya kimataifa na ligi kuu msimu ujao.

“Kocha wetu tayari tumemalizana na amewahi kufundisha klabu kubwa Afrika hivyo ana uzoefu ule ambao sisi tunautaka.

“Tumempa Baraka zote, Simba msimu huu tunataka kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa, mara zote tunaishia robo fainali sasa tunataka kutimiza ndoto yetu ya kwenda nusu fainali.

“Tulimfuatilia Manojlović kwa muda mrefu sana tukaona ana vigezo vyote vya kufundisha timu kubwa, tukamshusha Msimbazi na kumpa mkataba, msimu ujao utakuwa wa tofauti zaidi kwetu,” kilisema chanzo hicho.

Championi tulimtafuta Meneja wa Habari na Mwasiliano wa Simba, Ahmed Ally ili aweze kuzungumzia ishu hiyo alisema: “Ishu nzima ya kocha hazijafika kwenye dawati lango, waacheni kwanza viongozi wafanye kazi wakimaliza tutawatangazia Wanasimba.”

Previous articleVIDEO:KUMBE KICHAPO CHA SIMBA MBELE YA PRISONS KILIWAUMIZA
Next articleMTIBWA SUGAR KUCHEZA KAMA FAINALI LEO