Home International BAYERN MUNICH WANAKUJA NA JAMBO LINGINE

BAYERN MUNICH WANAKUJA NA JAMBO LINGINE

MSIMU wa 2021/22 haukuwa bora kwa Bayern Munich kama wengi ambavyo walitarajia licha ya kutwaa taji la Bundesliga kwa mara ya kumi mfululizo.

 Bayern Munich katika msimu wa 2021/22, walitolewa DFB Pokal dhidi ya Borussia Monchengladbach kwa mabao 5-0, huku Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiishia robo fainali wakiondoshwa na Villarreal.

 Licha ya Kocha Julian Nagelsmann kuwasajili Dayot Upamecano kwa euro 42.5m na Marcel Sabitzer (euro 15m), viwango vyao havikuridhisha kama ambavyo ilitarajiwa.

 Kwa maana hiyo, Bayern Munich wanatakiwa kufanya kazi hasa katika dirisha hili la usajili kwa kulitumia vyema.

ISHU YA KUMZUIA LEWANDOWSKI

Hatma ya Robert Lewandowski ndani ya Bayern Munich bado haijafahamika kutokana na ishu za mkataba wake uliobaki mwaka mmoja, staa huyo anataka kuondoka kikosini hapo baada ya kudumu hapo kwa miaka nane.

 Staa huyo alinukuliwa akisema: “Bado nina mwaka ndani ya mkataba, nimeomba ruhusa kwa ajili ya kuondoka.

 “Kwa sasa nafikiria kufanya uamuzi sahihi kutokana na hali ilivyo, lakini ninaamini klabu itapata fedha endapo nitauzwa, ingawa sitaki kulazimisha mambo.”

 Hivi karibuni, kumekuwa na taarifa zaidi kuwa huenda nyota huyo akaondoka kikosini hapo licha ya kwamba bado anahitajika kusalia. Kilichobaki ni kuona namna gani wanafanikiwa kumshawishi asiondoke.

 KUTUA KWA MANE

Tayari Bayern Munich wameshakamilisha usajili wa Sadio Mane ambaye amejiunga na timu hiyo wiki hii akitokea Liverpool.

 Winga huyo kwa sasa ana miaka 30, ni raia wa Senegal ambaye amekuwa akicheza kama mshambuliaji wa kati na pembeni, ndani ya Bayern Munich ataenda kushirikiana na kina Kingsley Coman na Serge Gnabry.

 USAJILI MWINGINE

Wakati dili la Mane likiwa limekamilika, Bayern Munich tayari walifanya usajili mwingine kuongeza nguvu kikosini hapo.

 Bayern imemsajili Ryan Gravenberch kwa euro 18.5m na Noussair Mazraoui aliyetua akiwa mchezaji huru.

 Gravenberch mwenye miaka 20, amekuwa mchezaji bora ndani ya Ulaya, anaonekana yuko bora kifiziki na huyo ataongeza nguvu katika eneo la kiungo hasa baada ya kuondoka kwa Marc Roca na Corentin Tolisso.

Previous articleRASMI:KOCHA MPYA SIMBA NI MSERBIA
Next articleHATIMAYE KAFIKA KOCHA SIMBA,YANGA YAMPA NABI MIAKA MIWILI