Home Sports ARSENAL WAINASA SAINI YA KIUNGO MSHAMBULIAJI

ARSENAL WAINASA SAINI YA KIUNGO MSHAMBULIAJI

KLABU ya Arsenal ya nchini Uingereza imefanikiwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji wa klabu ya FC Porto ya nchini Ureno Fabio Vieira (22).

Arsenal imekamilisha dili la kumsajili kiungo uyo kwa ada ya Paundi milioni 34 ambayo ni sawa na Shilingi Bilioni 96.9 za kitanzania ambapo itatoa Paundi milioni 30 kwanza halafu Paundi milioni 4 inayobaki itategemea na namna atakavyofanya vizuri katika kikosi hicho cha washika mitutu wa London.

Usajili wa Fabio Vieira unakuwa ni usajili wa tatu kwa Arsenal msimu huu, ambapo kikosi hicho cha Mikel Arteta kinajiandaa kutoa upinzani kwa msimu ujao wa ligi wa 2022/2023.

Hadi sasa Klabu ya Arsenal haijathibitisha usajili wa kiungo huyo mshambuliaji lakini tayari klabu ya FC Porto kupitia ukurasa wake rasmi wa klabu hiyo umethibitisha Vieira kutimkia Arsenal.

Vieira amefanikiwa kufunga mabao 6 katika michezo 15 aliyoanza msimu uliopita na jumla ya mabao 13 katika michezo 21 aliyocheza akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa ya Ureno chini ya umri wa miaka 21.

Arsenal bado inaendelea na harakati zake za kukamilisha dili la kumnasa mshambuliaji wa Manchester City na Timu ya Taifa ya Brazil Gabriel Jesus ili kuziba pengo la mshambuliaji wake aliyetimkia klabu yake ya zaman ya Olympique Lyonnais Alexandre Lacazette.

Previous articleISHU YA UFUNGAJI BORA MAYELE AFUNGUKIA
Next articleVIDEO:MSHAMBULIAJI HUYU TP MAZEMBE AINGIA ANGA ZA SIMBA