Home Sports MAKOCHA WAIGOMBEA SIMBA, CV ZA KUTOSHA ZATUMWA MSIMBAZI

MAKOCHA WAIGOMBEA SIMBA, CV ZA KUTOSHA ZATUMWA MSIMBAZI

MARA baada ya Simba SC kutangaza kuachana na kocha, Pablo Franco Martin, tayari baadhi ya makocha wameanza kuomba nafasi ya kufanya kazi ndani ya timu hiyo.

Taarifa ambazo Spoti Xtra limezipata ni kwamba, kocha wa kwanza kutuma wasifu wake akiomba mikoba ya Pablo kikosini hapo ni Brandon Truter raia wa Afrika Kusini.

Juzi Jumanne, Simba ilitangaza kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wa Pablo baada ya kushindwa kufikia malengo yaliyowekwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports na kufika nusu fainali michuano ya kimataifa.

Akizungumza na Spoti Xtra, meneja wa kocha huyo, Herve Tra Bi, alisema tayari wametuma CV zao ndani ya Simba na wanasubiri majibu kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo kuona uwezekano wa kuifundisha timu hiyo.

“Ni kweli tumetuma CV kwa ajili ya kupata nafasi ya kuifundisha Simba, Kocha Brandon Truter ni kocha mzoefu na soka la Afrika jambo ambalo ni kipaumbele kwa sasa kwa Simba katika sifa za kocha wanayemuhitaji.

“Tayari nimewasiliana na uongozi wa Simba na wameniambia juu ya vigezo vya kocha ambaye wanamuhitaji, nimeona huyu anawafaa,” alisema kiongozi huyo.

Brandon Truter kwa sasa ni kocha wa muda wa AmaZulu FC ya Afrika Kusini akiianza kazi hiyo Machi 27, 2022.

Kabla ya hapo, alikuwa Kocha Msaidizi wa Cape Town All Stars kuanzia Julai 1, 2017 hadi Novemba 30, 2017, kisha akakabidhiwa rasmi timu hiyo Desemba 1, 2017 hadi Juni 30, 2018.

Julai 1, 2018, alianza kuinoa Richards Bay FC, hadi Septemba 29, 2019. Kisha akatua Swallows FC kuanzia Septemba 30, 2019 hadi Novemba 28, 2021. Baada ya hapo, ndio ametua AmaZulu FC.

Previous articleHOROYA AC, RAJA CASABLANCA ZAMGOMBEA PABLO
Next articleVIDEO: MAMBO NI MOTO YANGA, WATANGAZA UCHAGUZI MKUU KUMPATA RAIS NA MAKAMU WAKE