MAPITO YA GEORGE MPOLE NA GUMZO LAKE KWA SASA

    KWA sasa gumzo kubwa kwenye Ligi Kuu Bara ni mshambuliaji George Mpole anayekipiga pale Geita Gold FC akiwa mzawa mwenye mabao mengi kwenye ligi msimu huu huku nafasi ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora kwa upande wake ipo kwa asilimia 60 hadi sasa.

    Mpole amehusika kwenye mabao 15 ya Geita Gold ambapo hadi sasa amefunga mabao 12 na pasi za mabao tatu akilingana na Fiston Mayele wa Yanga ambaye pia amehusika kwa idadi hiyo ya mabao ndani ya kikosi cha Wananchi.

    Kwa sasa kwenye vijiwe vya kidigitali gumzo kubwa ni Mpole na hatma yake pale Geita Gold tayari wengi wamemtabiria kuibukia Kariakoo kutokana na kiwango anachokionyesha hadi sasa.

    Mpole hakuwa mchezaji tishio msimu uliopita akiwa na kikosi cha Polisi Tanzania jambo lililopelekea aachwe na Geita Gold wakapita naye na sasa amegeuka lulu na hakuna timu ambayo haitamani kuwa na mshambuliaji wa aina yake.

    Akiichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza katika michezo miwili alifanikiwa kufunga bao na kutoa pasi moja ya bao.

    Ukiangalia kwa hali inavyoendelea hivi sasa ni ngumu sana Geita Gold kumzuia Mpole asiondoke pale Nyankumbu. Shida siyo Mpole kuondoka shida ni atakapokwenda je atafanikiwa? Kwani hapo nyuma wamepita wachezaji vijana wengi walioonyesha kiwango bora na walipofika Kariakoo mambo yaliwaendea kombo.

    Mnamkumbuka Adam Salamba wa Lipuli? Salamba ni mmoja ya wachezaji ambao walitabiriwa kufika mbali kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha akiwa na kikosi cha Lipuli jambo lililowaingiza vitani Simba na Yanga kuwania saini yake na Simba walifanikiwa kumnasa lakini alishindwa kufikia matarajio ya Wanasimba wengi kwani hakuwa Salamba yule waliyemwona Lipuli.

    Siyo Salamba pekee kiliibuka kizazi cha washambuliaji wazawa kama Mohammed Rashid, Marcel Kaheza, Salim Aiyee na wengine wengi ambao tuliwatarajia kuja kurithi mikoba ya akina John Bocco pale Stars lakini hadi sasa hawajulikani wanafanya nini.

     Kaheza hana uhakika wa namba pale Ruvu Shooting wakati Mohammed Rashid hana uhakika wa namba kwenye kikosi cha JKT Tanzania kinachoshiriki Championship kwa upande wa Salim Aiyee hata sielewi nini kilimkuta.

    Hali hii inafanya nimtazame George Mpole kwa jicho la tatu je kama atafanikiwa kuja Kariakoo ataweza kuvunja mwiko huu wa wachezaji wanaowika kwenye timu za kawaida kushindwa kutamba Kariakoo? Je ni John Bocco mpya kwenye kikosi cha timu ya taifa?

    Majibu ya maswali haya yapo kwenye kurasa za kitabu chake yeye ndiyo anaweza kutupa majibu sahihi ya kile ambacho tunakiwaza.

    Kwa sasa Geita Gold ni miongoni mwa timu ambazo zinapambana kuwania nafasi nne za juu kutokana na mabadiliko makubwa yaliyofanyika ndani ya kikosi hicho na kama watafanikiwa kumaliza kwenye nafasi hizo wana nafasi kubwa ya kushiriki michuano ya kimataifa ni sehemu nyingine ya Mpole kuuonyesha Ulimwengu kuwa Tanzania hatuna Kelvin John na Mbwana Samatta pekee.

    Kama hawatafanikiwa kumaliza katika nafasi nne za juu sioni nafasi ya Geita Gold kumbakisha na hii inatokana na aina ya mikataba ambayo timu zetu wamekuwa wakiwapa wachezaji wao, ni aghalabu sana kukuta mchezaji anapewa mkataba wa miaka mitatu hadi minne hii inatokana na wachezaji wetu kutokuwa na mwendelezo (consistency).

     Inakuwa ngumu kwa wao kupewa mikataba mirefu hivyo inapotokea wanafanya vizuri timu zao zinajikuta zikikosa mapato ya kutosha kwani wengi huondoka wakiwa huru bila mkataba wowote.

    Jicho la Fred Felix Minziro liliona kitu ndani ya George Mpole na sasa Geita wanafaidika na matunda ya ubora wake uwanjani, uwezo wa kufunga mabao kwa staili zote, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na uwezo wa kutengeneza mabao hizi ni sifa alizonazo George Mpole suala ni ataweza kuyafanya haya kama atakuja Kariakoo.

    Huu ni muda wake kupita kwenye kurasa za akina Adam Salamba, Mohammed Rashid na Marcel Kaheza ili kujitengenezea ramani yake ambayo haitampoteza kama akija Kariakoo.

    Previous articleMUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMAPILI
    Next articleTEN HAG ATUMIWA UJUMBE NA RONALDO