Home International LIVERPOOL INAKARIBIA MAKOMBE 4 KWA MSIMU HUU

LIVERPOOL INAKARIBIA MAKOMBE 4 KWA MSIMU HUU

LIVERPOOL baada ya kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi, sasa kuna uwezekano wa miamba hiyo ya Anfield kutwaa makombe manne makubwa ‘quadruple’ ndani ya msimu mmoja. Itakuwa ni historia na rekodi ambayo haijawahi kuwekwa England.

Liverpool iliichapa Villarreal 3-2 ugenini juzi nchini Hispania, na kuwaondoa vijana hao wa kocha Unai Emery kwa jumla ya mabao 5-2.

Sasa baada ya kutinga fainali, Liverpool ina uwezekano wa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England ambapo ipo nyuma ya vinara Man City kwa tofauti ya pointi moja, Kombe la FA (itacheza fainali dhidi ya Chelsea Mei 14) na tayari imeshatwaa ubingwa wa Kombe la Ligi kwa kuichapa Chelsea katika mchezo wa fainali uliochezwa Februari 27, 2022.

Kuna timu tisa ziliwahi kutwaa makombe matatu ya ligi, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya (zamani Kombe la Ulaya), lakini ni timu moja tu ndiyo ambayo imewahi kutwaa makombe yote manne makubwa. Je, Liverpool inaweza kuwa timu ya pili kufanya hivyo?

Liverpool inaonyesha dalili zote kuwa mwaka huu inaweza kufanikiwa hivyo, lakini inaiombea Man City itoke sare hata mchezo mmoja dhidi ya Newcastle (nyumbani), Wolves (ugenini), West Ham (ugenini) au Aston Villa (nyumbani) huku yenyewe ikitakiwa kushinda mechi zote dhidi ya Tottenham (nyumbani), Aston Villa (ugenini), Southampton (ugenini) na Wolves (nyumbani) ili iweze kutwaa ubingwa wa Premier.

Tayari Liverpool imetwaa Kombe la Ligi kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 11-10 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu.

Liverpool inaonekana haifungiki kwa sasa, na uwezekano wa kutwaa makombe manne unaweza ukazimishwa na suala la Manchester City kushinda mechi zote zilizobaki za Premier.

Mechi ya mwisho ya ligi itakuwa ni Mei 22, yaani siku sita kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Manchester United ndiyo timu pekee ya England hadi sasa iliyoshinda makombe matatu makubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (zamani Kombe la Ulaya), Kombe la Ligi na Kombe la FA, ilikuwa ni msimu wa 1998/99. United ilishindwa kutwaa makombe manne baada ya kutolewa katika hatua ya robo fainali kwenye Kombe la Ligi.

Mara pekee Liverpool ilipokaribia mafanikio hayo ilikuwa ni msimu wa 1976/77, waliposhinda ligi na kombe lao la Ulaya (Ligi ya Mabingwa sasa) lakini ikapoteza 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United.

Celtic ya msimu wa 1966/67 ndiyo timu pekee hadi sasa iliyowahi kutwaa makombe manne ndani ya msimu, ya Kombe la Ulaya (kwa sasa Ligi ya Mabingwa Ulaya), ligi ya ndani, Kombe la FA na Kombe la Ligi ndani ya msimu mmoja.

Previous articleRASMI: CHELSEA YAUZWA KWA MMILIKI MPYA, MWISHO WA ENZI ZA ROMAN ABRAMOVICH
Next articleNYOTA MAN UNITED AWA MUUZA SAA