MBEYA Kwanza yenye maskani yake Mbeya kwa sasa sio ya kwanza kwa timu ambazo zina maskani yake kwenye mkoa huo wenye madhari ya kijani.
Kwa sasa kwenye msimamo inaburuza mkia ikiwa imekusanya pointi 14 baada ya kucheza mechi 19.
Safu ya ushambuliaji ya Mbeya Kwanza imetupia mabao 14 ikiwa imeshinda mechi 2 pekee za ligi.
Kwa timu za Mbeya iliyo ya kwanza kwa sasa ni Mbeya City ambayo ipo nafasi ya tano na pointi 25 baada ya kucheza mechi 19.
Ile kasi ya kushinda na kupata pointi kwenye mechi zao za ligi kwa sasa nayo imepungua kwa kuwa mchezo wao uliopita dhidi ya Geita Gold ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Mtupiaji alikuwa ni George Mpole ambaye amefikisha mabao 9 akiwa ni namba moja kwa utupiaji kwa wachezaji wa Geita Gold na ni namba tatu kwa watupiaji wote kwenye ligi.
Tanzania Prisons wao pia wanajikongoja lakini kwa timu ambazo zinatokea Mbeya yenyewe ni namba mbili ikiwa nafasi ya 15 na ina pointi 16 kibindoni.
Ikumbukwe kwamba nafasi ya 15 na 16 ni ile ya hatari kwa timu kuweza kushuka moja kwa moja na kushiriki Championship ambayo nayo ushindani wake msimu huu umekuwa ni mkubwa.
Aprili 6 ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Biashara United mchezo uliochezwa Uwanja wa Karume, Mara.
Pia nyota wake Enock Jiah atakosekana kwenye mechi mbili kwa kuwa alionyeshwa kadi nyekundu hivyo ameshavuruga hesabu za kocha kwa mechi zijazo za ligi.