Home International KIBAO KUMPONZA WILL SMITH,TUZO YAKE YAJADILIWA

KIBAO KUMPONZA WILL SMITH,TUZO YAKE YAJADILIWA

LICHA ya staa mkubwa wa Hollywood, Will Smith kuomba msamaha jukwaani baada ya kumzaba kofi mchekeshaji Chris Rock, staa huyo pia ametumia akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuendelea kuomba radhi, safari hii akimuomba pia radhi Rock kwa kitendo alichomfanyia.

Will Smith ameandika:“Vurugu katika namna yake yoyote ni sumu na hubomoa. Tabia yangu usiku uliopita katika tukio la utoaji wa tuzo haikubaliki na haisameheki.

“Utani kuhusu mimi ni sehemu ya kazi yangu lakini utani kuhusu ugonjwa wa mke wangu ulivuka mipaka na kunifanya nishindwe kudhibiti hisia zangu.

“Napenda kuomba radhi hadharani kwako Chris. Nilitoka nje ya mstari na nilikosea. Najisikia vibaya kwamba tukio hilo limeenda tofauti na mipango ya jinsi ninavyotaka kuwa.

“Hakuna nafasi ya vurugu katika dunia iliyojawa upendo na huruma,” aliandika Smith.

Pia ameomba radhi kwa mara nyingine kwa waandaaji wa tuzo hizo na familia ya Williams ambayo kupitia filamu waliyoitengeneza kuhusu maisha yao, ndiyo Smith aliyopatia tuzo.

Bado Rock hajajibu chochote kuhusu msamaha huo wala hajatoa maoni yoyote lakini wanaharakati mbalimbali wanaendelea kupaza sauti wakitaka staa huyo anyang’anywe tuzo hiyo kwa kuonesha tabia mbovu hadharani.


Smith alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Oscars katika kipengele cha mwigizaji bora wa mwaka, kupitia filamu ya King Richard ambayo ameigiza kama Richard Williams, baba wa nyota wa mchezo wa tenisi duniani, Venus na Serena Williams, ikiwa ni mara yake ya kwanza kupata tuzo hiyo kubwa duniani.

Tukio la kumzaba kofi Rock, ambalo lilinaswa na kurushwa mubashara duniani kote kutokea katika Ukumbi wa Dolby Theatre, Hollywood nchini Marekani, limewakasirisha waandaaji wa tuzo hizo ambapo inaelezwa kwamba mjadala mkali umefanyika kumjadili Smith kama anastahili kuendelea kubaki na tuzo hiyo.

Baada ya kukabidhiwa tuzo yake, Will Smith aliutumia muda wa kutoa salamu za shukrani, kuwaomba radhi wote waliokasirishwa na kitendo cha kumpiga kibao Rock akiwa jukwaani na kueleza kwamba lilikuwa ni tukio ambalo haliwezi kusameheka kwa urahisi.

Sababu kubwa iliyomkasirisha Will Smith mpaka akafikia hatua ya kufanya tukio hilo ambalo halikutarajiwa, ni baada ya mshereheshaji huyo ambaye pia ni mchekeshaji, kumtania mke wa Will Smith, Jada Pinkett Smith kuhusu mtindo wake wa kunyoa nywele zote kichwani.

Previous articleTAIFA STARS KAZINI LEO,FEI TOTO KUIKOSA SUDAN
Next articleMKATABA WA NBC NA TFF KUWA NA TIJA KWA FAMILIA YA MICHEZO