KOCHA RS BERKANE AIHOFIA SIMBA KIMATAIFA, ATOA ANGALIZO

BAADA ya kuzitazama rekodi zake anapocheza na Simba, Kocha Mkuu wa RS Berkane, Florent Ibenge, amekiri
kukutana na upinzani mkali dhidi ya timu hiyo katika michuano ya kimataifa.

Ibenge amekutana na Simba mara nne katika michuano ya kimataifa wakati alipokuwa akiinoa AS Vita ya DR Congo
ambapo katika michezo hiyo amepoteza mitatu na akishinda mmoja.

Ibenge kwa sasa akiwa kocha mkuu wa RS Berkane ya nchini Morocco, anatarajiwa kukutana na Simba katika
mchezo wa Kundi D la Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Februari 27, nchini humo, ambapo timu hiyo imetoka kupoteza katika mchezo uliopita kwa mabao 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas.

 Ibenge amesema kuwa, rekodi zake dhidi ya Simba hazina matokeo mazuri
lakini sio sababu ya wao kushindwa kupata matokeo kwa kuwa wanayo kila sababu ya kupambana na kutafuta matokeo mazuri mara baada ya kupoteza katika mchezo uliopita wakiwa ugenini nchini Ivory Coast.

“Ni kweli rekodi yangu dhidi yao si nzuri lakini sio sababu ya sisi kufeli dhidi yao, kuna nafasi nzuri ya kupambana dhidi yao, tumetoka kupoteza katika mchezo uliopita tukiwa ugenini nchini Ivory Coast, hivyo tunatakiwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

“Kwa jinsi ambavyo ilivyo ni lazima tupate matokeo mazuri nyumbani kwa kuwa ugenini sio salama, kila timu imepanga kupata matokeo mazuri nyumbani, Simba wamepata matokeo tayari nyumbani na ugenini na hiyo ni faida kwao, ndio maana utaona kuwa wanaongoza kundi,” amesema kocha huyo.