KOCHA AZAM FC ATOA NENO HILI LA MATUMAINI

ABDI Hamid Moallin amesema kuwa mashabiki wa Azam FC watajivunia kitu kizuri na bora kutoka kwake baada ya kukabidhiwa rasmi timu hiyo iliyo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na pointi zake 21.

Moallin amesaini dili la miaka mitatu Jana Januari 25 ambapo awali alikuwa ni Kaimu Kocha Mkuu baada ya kurithi mikoba ya George Lwandamina kwa muda aliyebwaga manyanga.

Kocha huyo ameweka wazi kwamba anajua mashabiki wanahiitaji ushindi na timu hiyo imekuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu na mashabiki jambo ambalo analitambua na watafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

“Ninajua kwamba mashabiki wanapenda matokeo mazuri na wamekuwa pamoja nasi kwenye mechi ambazo tunacheza hivyo hakuna namna ambayo ninaweza kusema ni zaidi ya furaha pamoja na matokeo mazuri.

“Jambo lingine ni namna ya uchezaji ambapo tutakuwa na tofauti kwenye mbinu na namna ya kucheza hili litatufanya tuweze kuwa kwenye ubora na kupata kile ambacho tunahitaji. Kwangu ni furaha kuwa hapa,”.

Ni Yanga ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 35 kibindoni na hawajapoteza mchezo kwenye mechi 13 ambazo wamecheza msimu wa 2021/22.