TANZANITE YAITULIZA ETHIOPIA KOMBE LA DUNIA

TIMU ya taifa ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake chini ya miaka 20, ‘Tanzanite’ jana iliweza kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar na ulishuhudiwa na mashabiki wengi waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.

Dakika 45 za mwanzo ngoma ilikuwa ngumu kwa timu zote kutoshana nguvu na mbinu ya Tanzanite ilikuwa kujibu kipindi cha pili ambapo waliweza kupata bao la ushindi.

Ni kazi ya Christer Bahera ambaye aliwamaliza Ethiopia ilikuwa ni dakika ya 64 na bao hilo lililindwa katika dakika 26 zilizobaki na kuipa timu ya Tanzania ushindi.

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzanite, Bakari Shime amesema kuwa wamepata nafasi nyingi lakini wametumia nafasi moja.

“Kipindi cha kwanza tulipata nafasi nyingi lakini tulishindwa kuzitumia kutokana na wachezaji wetu kushindwa kupata matokeo.

“Lakini mwisho wa siku tumeweza kupata ushindi hilo ni jambo la furaha kwetu na shukrani kwa mashabiki ambao walijitokeza kwenye mchezo wetu na maandalizi yanafuata kwa ajili ya mchezo ujao,”.

Kikosi kwa sasa kimeelekea Karatu kwa ajili ya kuweza kuweka kambi kuelekea kwenye mchezo wa marudio unaotarajiwa kuchezwa mwezi ujao wa Februari.