MUKOKO AINGIA ANGA ZA SIMBA,ATAJWA KUTOKUWA NA FURAHA

IMEELEZWA kuwa kiungo mkabaji ndani ya kikosi cha Yanga, Mkukoko Tonombe amegomea mkataba mpya kwa ajili ya kuendelea kuitumikia timu hiyo.

Mukoko ndani ya Yanga kwa sasa amepoteza nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza msimu huu kutokana na
uwepo wa Khalid Aucho na Yanick Bangala ambao wamesajiliwa msimu huu.

Wakati Mukoko akiwa kwenye hatihati kubaki Yanga, taarifa kutoka Simba zinadai kwamba, tayari uongozi wa klabu hiyo umeanza kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo huyo ambaye mkataba wake umebaki miezi sita kabla ya kumalizika.

Kwa sasa Simba inasaka kiungo mkabaji mara baada ya Tadeo Lwanga kuwa na majeraha ya mara kwa
mara hivyo wanasaka mbadala wake.

“Simba kwa sasa inatafuta kiungo mkabaji wa kuja kuchukua nafasi ya Tadeo Lwanga na tayari uongozi wa Simba unafahamu kuwa Mukoko Tonombe mkatabawake na Yanga umebaki miezi sita, hivyo lolote linaweza kutokea.

“Mukoko ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kucheza kikosi cha timu yoyote katika ligi yetu, hivyo kuwa naye katika kikosi ni moja ya kuwa na silaha nzuri ya kivita ambayo muda wowote ipo tayari kwa mapambano,” kilisema chanzo hicho.

Naye rafiki wa karibu wa Mukoko Tonombe kutoka DR Congo ambaye hakutaka jina lake kutajwa, alisema:
“Mukoko Tonombe kwa sasa hana furaha ndani ya Yanga, sio kama ilivyokuwa hapo awali, hii inatokana na yeye kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara na hataki kuongoza mkataba akihitaji changamoto sehemu nyingine.

“Yeye mwenyewe alikuwa na malengo ya kuisaidia Yanga, lakini kwa sasa hali imebadilika na aliniambia
kuwa AS Vita wanajaribu kumrudisha nyumbani, lakini kuna ofa amepokea kutoka timu kubwa kutoka Tanzania, hivyo ngoja tuone nini kitatokea.”