>

2022 IKAWE BORA NA YENYE MAFANIKIO PIA

2021 kwa sasa inahitaji kutuacha kwa kuwa tayari yale mapigano yote yamefanyika na wapo ambao wameambulia maumivu na wengine ilikuwa ni furaha kwao.

Kwenye ulimwengu wa mpira tumeona namna ushindani ulivyokuwa kwa kila timu kupambana kusaka ushindi hilo ni jambo la msingi na ni muhimu kuendelea kufanyika.

Pia kwenye Ligi ya Wanawake Tanzania nayo pia imeanza kurindima ikiwa ni ishara nzuri kwamba bingwa mwingine anatafutwa kwa ajili ya msimu wa 2021/22 na inawezekana kikubwa ni ushindani na kila timu kusaka ushindi.

Hakuna ambaye alikuwa anapenda kwa mwaka 2021 kuweza kuambulia maumivu ama kushindwa kufikia malengo ambayo yalikuwa yameandikwa lakini ni sehemu ya mchezo.

Kitu cha msingi kwa sasa kila mmoja kutazama namna ambayo kwake ni bora katika kutimiza majukumu bila kumuumiza mwingine kwa kuwa hakuna namna ya kukwepa matokeo ya uwanjani.

Wachezaji katika mechi za ligi imeonekana kwamba wamekuwa wakikamiana na wakati mwingine wapo ambao wamekuwa wakiumizana kwa bahati mbaya ama kwa makusudi lakini hakuna ambaye anaweza kuwa na ushahidi wa moja kwa moja.

Msingi kwa wachezaji kwenye mechi ni kusaka ushindi na wanatumia akili nyingi uwanjani na wakati mwingine wanatumia nguvu kwa sababu kwa kutumia nguvu hivyo msingi uwe kwenye mabadiliko kwa mwaka mpya kufanya kile kilicho bora zaidi.

Imani ni kwamba kwa mwaka 2021 kuna mazuri ambayo timu zimefanya katika hilo pongezi mnastahili na pale ambapo mlikwenda tofauti ni muhimu kuweza kujipanga upya.

Kwa ambazo zinashiriki Championship nazo pia zina mipango yake hasa kufikiria kupanda ligi hilo ni jambo la msingi muhimu kupambana bila kukata tamaa.

Basi kinachotakiwa kwa sasa ni kuwa makini kwenye kila mechi na wachezaji wawe makini kuwalinda wachezaji wengine.

Mlinzi wa kwanza wa mchezaji uwanjani ni mchezaji mwenyewe hivyo kwa wakati huu rai yangu ni kuona kwamba kila mchezaji anakuwa mlinzi.

Iwe tofauti kwa mwaka 2022 na kila timu iweze kufanya vema katika kupambana kusaka ushindi na imani yetu ni kwamba kila timu inahitaji kufikia malengo ambayo imejiwekea.

Kikubwa kinachohitajika ni maandalizi makini na kila mmoja kutimiza majukumu yake kwa wakati sahihi jambo hili litaongeza ushindani na kuleta matokeo mazuri.

Mara nyingi tumeshuhudia timu kuanza kuonyesha ushindani mkubwa kwenye mechi zao za awali ama msimu wa kwanza mwisho wa siku zinaangukia pua msimu unaofuata.

Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mpango makini na ukweli ni kwamba kupanda ni rahisi na kushuka ni rahisi pia lakini ukishashuka kurudi huku juu huwa inakuwa ngumu.

Hivyo kwa kuwa ni mwaka mwingine basi ni wakati wa kila mmoja kuweza kuangalia hesabu mpya katika kutimiza malengo.

2022 ikawe ni wakati wa kutimiza malengo na ukawe ni mwaka wa mafanikio kwa timu zote hasa ambazo zinapambana kwa hali na mali huku wachezaji wao wakipaswa kuwa makini.

Imani yangu ni kwamba zile ambazo zimepanda zinatambua kwamba kuna ushindani mkubwa kwenye ligi na wanatambua pia lipo suala la kushuka.

Tunataka kuona timu ikipanda kwenye ligi iwe na uwezo na vigezo vya kuhimili mikikimikiki ya huku kwani hakuna kuzubaa ni mwendo wa kukimbizana.

Siri ya kufanya vizuri kwenye mechi za ligi ni maandalizi mazuri kwa wakati huu ni lazima kila mmoja awe tayari kwa ajili ya mechi zote ambazo atacheza kwa msimu ujao ambao nao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Jambo lingine ambalo wachezaji wanapaswa kutambua ni kwamba nidhamu ni suala la lazima kwao ikiwa wanahitaji kufikia mafanikio yao kila wakati.

Itawafanya waweze kuwa bora muda wote ndani ya uwanja na kuyafikia mafanikio yao pamoja na yale ya timu kiujumla kwa kuwa inawezekana kufanya hivyo.

Ikiwa watashindwa kuwa na nidhamu nje ya uwanja na ndani ya uwanja inaweza kuwafanya washindwe kupata hata timu za nje ya nchi.

Kila kitu kwenye soka kinahitaji nidhamu na 2022 iwe bora zaidi na kila la kheri ya mwaka mpya.