USAJILI UZINGATIE RIPOTI YA BENCHI LA UFUNDI

HEKAHEKA za usajili wa dirisha dogo ndani ya Ligi Kuu Bara zimeanza huku timu nyingi zikianza mikakati ya kuviboresha vikosi vyao kuelekea mzunguko wa pili ili ziweze kufanya vizuri kwenye ligi na michuano mingine ambayo watashiriki.

 

Kipindi hiki timu zinapaswa kuwa makini katika kuhakikisha wachezaji ambao watasajiliwa waendane na mahitaji ya benchi la ufundi na usiwe usajili wa kukurupuka au wa kuwafurahisha mashabiki.

Ni kipindi ambacho kila kiongozi au mtu mwenye ushawishi ndani ya timu atakuja na jina la mchezaji wake mezani na kulazimisha asajiliwe pasi na kuangalia kama mchezaji huyo ana tija ndani ya kikosi au la.

 

Kuna kasumba ambayo imekuwa ikiendelea kwenye ligi yetu hususan kwenye timu kubwa na zile za madaraja ya kati ambazo zinakuwa na bajeti kubwa kuelekea kipindi cha usajili ambapo usajili umekuwa ukifanyika kiholela bila kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi.

 

Jambo la kusikitisha ni pale mambo yanapogeuka makocha wanajikuta wakibebeshwa zigo la lawama ambalo hawakustahili hata kidogo, hivi karibuni tumeona timu kadhaa zikiingia hasara ya kusajili wachezaji kwa fedha kubwa ambao wameshindwa kuonyesha chochote uwanjani na mwisho wa siku mikataba yao imevunjwa huku timu zikipata hasara kubwa.

 

Ni lazima uwepo utaratibu wa kufanyika kwa tathmini ya kina kabla ya usajili wa wachezaji kufanyika, ni lazima timu zijiwekee vigezo (standards) ambazo mchezaji anapaswa kuzifikia ili aweze kusajiliwa na timu husika, kwa mfano mchezaji lazima awe kwenye timu ya taifa kwa wachezaji wa kigeni ili kuondoa lundo la wachezaji mizigo ndani ya timu.

 

Ni wazi makocha watakuwa wameandaa ripoti zao kuelekea mzunguko wa pili, kuona ni mchezaji gani anahitajika ndani ya kikosi na nani hahitajiki kikosini na si viongozi kuingilia mipango ya benchi la ufundi na kujikuta wanasajili wachezaji kwa mapendekezo yao wenyewe.

 

Siyo muda wa kiongozi kuonyesha ufahari wake katika kufanya usajili ambao ni kinyume na matakwa ya benchi la ufundi kwa ajili ya kutafuta umaarufu kwa mashabiki ambao hauna tija yoyote, na baadaye mambo yanapokuwa magumu makocha wanajikuta wakiadhibiwa kwa uzembe wa watu wachache.

 

Usajili wa mihemko hiki siyo kipindi chake, bali jikiteni katika kufanya sajili ambazo zitafanya vikosi vyenu kuwa tishio na si kutafuta visingizio hapo baadae baada ya kufeli kwenye mipango yenu. Kuna timu kadhaa tumeona zimefanya usajili wa mihemko na mwisho wa siku wanajikita kwenye visingizio ambavyo havina msingi baada ya wachezaji wao kufeli.

 

Mwisho huu siyo muda wa kufanya usajili wa kukomoana, kuona mchezaji anatakiwa na timu fulani na nyie mkajikuta mnaingilia kati dili hilo licha ya kuwa mchezaji hayupo kwenye mipango yenu, usajili uzingatie mahitaji ya benchi la ufundi kwa ustawi wa timu zenu.