SIMBA BADO WACHEZAJI WANAUMWA,MAZOEZI WAMEFANYA SIKU MBILI

WAKATI leo kikosi cha Simba kikiwa na kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya KMC ambao ni wenyeji bado wachezaji wa timu hiyo wapo ambao wanaumwa.

Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Simba, Thiery Hitimana amesema kuwa bado wachezaji hawajawa fiti kwa asilimia 100 kutokana na homa ambayo walikuwa nayo.

Ikumbukwe kwamba Desemba 18 Simba ilikuwa na kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Kagera Sugar lakini mchezo huo uliahirishwa kwa kuwa wachezaji na benchi la ufundi wa Simba walikuwa wanaumwa homa na mafua.

Thiery amesema hayo muda mfupi kabla ya mchezo kuanza kupitia mahojiano ya moja kwa moja na Azam TV ambao watarusha mchezo huo mubashara kutoka Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

“Tumepata nafuu lakini hatujawa sawa kwa asilimia 100 kwa sababu ugonjwa wa mafua huwa hauwez kupona moja kwa moja ndani ya siku tatu lakini wachezaji wapo tayari.

“Pia wachezaji wamefanya mazoezi kwa muda wa siku mbili na leo ni siku ya tatu bado tuna kazi ya kufanya hasa kwa upande wa utayari wao na mchezo tunatambua kwamba utakuwa mgumu,”amesema Thiery, Kocha Msaidizi wa Simba.