>

NYOTA HAWA WATATU KUONDOKA AZAM FC

JUMLA ya wachezaji nyota  watatu wanatarajiwa kuondoka katika kikosi cha Azam FC kwenda katika timu ya taifa ya Zimbabwe kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON).

Wachezaji hao ni beki wa kushoto, Bruce Kangwa, kiungo Never Tigere na mshambuliaji Prince Dube.Nyota hao huenda wakakosekana katika michezo baadhi ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA kutokana na kuwepo katika majukumu ya timu ya taifa.

Kwa mujibu wa mtandao wa nchini Zimbabwe, wachezaji hao wameitwa katika kikosi cha awali kuelekea michuano ya AFCON itakayoanza Januari 9 hadi Februari 6, 2022 nchini Cameroon.

Mastaa hao wa Azam,wanatarajiwa kuingia kambini hivi karibuni kwa ajili ya mchujo wa mwisho utakaowawezesha kuwepo sehemu ya kikosi cha Zimbabwe kitakachokwenda Cameroon katika michuano hiyo.

Ofisa Habari wa Azam FC, Thabiti Zakaria, alithibitisha hilo kwa kusema: “Ni kweli wachezaji hao wameitwa katika kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Zimbabwe, hivyo muda wowote watajiunga nayo.”