YANGA rasmi imemalizana na mashine tano ambazo muda wowote zitatambulishwa mara baada ya kufikia muafaka mzuri katika usajili wa dirisha dogo.
Dirisha hilo lilifunguliwa mapema Desemba 16, mwaka huu na Yanga imepanga kufanya usajili mkubwa katika kukiimarisha kikosi chao.
Wakati wakipanga kusajili wachezaji hao watano, pia wamepanga kuwaacha baadhi ya wachezaji wake Ditram Nchimbi, Paul Godfrey ‘Boxer’, Ramadhani Kabwili na Adeyum Saleh.
Taarifa ambazo tumezipata mashine hizo walizomalizana nazo mawinga wawili ambao ni Chico Ushindi kutoka TP Mazembe ya DR Congo atakayekuja kusaidiana na Jesus Moloko na Denis Nkane wa Biashara United atakayekuwa na kibarua cha kumuondoa mkongwe Said Ntibanzokiza ‘Saido’.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, uongozi umefanikisha usajili wa kiungo mchezeshaji wa Azam FC, Salum Aboubakri ‘Sure Boy’ ambaye tayari ameomba kuondoka katika timu hiyo atakayekuja kupambania namba na Mganda, Khalid Aucho.
Aliwataja wengine ni makipa wawili ambao ni Mohammed Makaka wa Ruvu Shooting atakayekuja kuchukua nafasi ya Djigui Diarra na Abdallah Msherry anayeidakia Mtibwa Sugar anayekuja kuchukua nafasi ya Ramadhani Kabwili kama kipa wa timu ya vijana.
“Uongozi umemalizana na wachezaji watano hadi hivi sasa, lakini pia uongozi upo katika hatua za mwisho za kukamirisha usajili wa mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Crispin Ngushi.
“Ngushi huenda akasajiliwa naye hivi karibuni kwani yupo katika mazungumzo, kocha Nabi ndiyo
anaonekana kuvutiwa na usumbufu anaowapa mabeki wa timu pinzani.
“Wachezaji hao waliomalizana na viongozi wote wamesaini miaka miwili, isipokuwa Chico yeye atajiunga na Yanga kwa mkopo kutoka Mazembe, lakini atasini mkataba wa kudumu mara baada ya mkataba wake kumalizika katika klabu yake,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia ishu ya usajili pale Yanga, Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Fredrick Mwakalebela alisema; “Kila kitu kuhusu usajili kipo kwa kocha Nabi ambaye ndiye anapendekeza nani asajiliwe na nani aachwe.”
STORI NA CHAMPIONI JUMATANO | GPL