RASMI Azam FC imekubali kumuachia kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na sasa yupo huru kujiunga na Yanga katika usajili huu wa dirisha dogo.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kiungo huyo awasilishe ombi la kuvunja mkataba huo mara baada ya kusimamishwa na viongozi wa Azam.
Sure Boy alisimamishwa pamoja na wachezaji wenzake wawili, Mudathiri Yahya na Aggrey Morris kwa utovu wa nidhamu.
Mkuu wa Fedha wa Yanga, Haji Mfikirwa, alithibitisha kufikia muafaka mzuri na Azam baada ya kukubaliana
pande zote mbili kumsajili Sure Boy.
“Sure Boy tumekubaliana, tumeafikiana, kuongeza dozi,” alisema Mfikirwa ambaye amerejeshwa katika cheo cha mkuu wa fedha baada ya Senzo Mazingiza kuteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Yanga.
Azam kupitia Ofisa Habari, Thabiti Zakaria, alisema kuwa wamekubali ombi la kiungo huyo alilowasilisha ili kuvunja mkataba.
“Sure Boy amewasilisha rasmi barua ya kuomba kuvunjiwa mkataba, na uongozi wa timu yetu umekubali kumuachia kwenda kutafuta maisha kwingine.
“Anachotakiwa kufanya ni kwenda kuchukua barua ya kumruhusu kuondoka katika ofisi ile ile aliyopeleka barua,” alisema Thabiti.
Kwa upande wa meneja wa kiungo huyo, Heri Mzozo, alitibitisha Sure Boy kujiunga Yanga kwa kusema: “Ipo
wazi kabisa, Sure Boy anakwenda Yanga, masuala yote ya msingi hadi kufikia leo (jana) yameisha.
“Hiyo ni baada ya viongozi wake wa Azam kumpa baraka zote, amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga.”