USAJILI unaofanywa na Simba na Yanga kipindi hiki cha dirisha dogo ni umafia mtupu kwani hakuna ambaye
anataka kuona mchezaji wake akiporwa.
Katika kuhakikisha kila timu inafikia malengo yake, imefahamika kuwa, Jumapili Yanga imemshusha kimyakimya kiungo mshambuliaji kutoka nchini DR Congo tayari kwa ajili ya kusaini mkataba wa kukipiga Jangwani.
Taarifa zimeeleza kuwa kiungo huyo ambaye kwa sasa jina lake wameamua kulificha kuogopa kuporwa na wapinzani, alitua Jumapili asubuhi na kupelekwa kwenye moja ya hoteli kubwa na ya kifahari iliyopo Posta, Dar es Salaam.
Mtoa taarifa huyo alisema kiungo huyo Jumatatu alitarajiwa kukutana na mabosi wa Yanga mara baada ya timu kurejea Dar es Salaam ikitokea Sumbawanga kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons.
“Jumapili asubuhi alitua nchini kiungo mshambuliaji kutoka DR Congo aliyekuja kwa ajili ya kumalizana na uongozi wa timu yetu.
“Kama unavyofahamu Yacouba (Songne) yupo nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti, hivyo huyo jamaa ndiye atachukua nafasi yake na muda wowote kuanzia sasa atasaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alipoulizwa kuzungumzia hilo, alisema kwa sasa hana taarifa za ujio wa kiungo huyo.