TANZANIA PRISONS YAZIPIGIA HESABU POINTI ZA YANGA

KUELEKEA mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga, Tanzania Prisons wametamba kuwa wapinzani wao hawawatishi na watahakikisha wanavunja rekodi yao ya kutofungwa tangu kuanza kwa msimu huu. Mchezo huo wa ligi kuu unatarajiwa kupigwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.

 Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons, Shaban Kazumba alisema: “Tunamshukuru Mungu tunaendelea na mazoezi kuelekea kwenye mchezo wetu wa ligi unaofuata dhidi ya Yanga japo kuna mvua kidogo

“Kama tulivyopeleka maumivu ya mabao matatu kwa Kitayosce kwenye mashindano ya FA kwa sasa tunajipanga ili kupeleka tena maumivu hayo kwenye mchezo huo unaofuata.

“Tunajua Yanga wana timu nzuri na wana historia kubwa lakini hilo halitutishi kwani hata sisi tuna rekodi ya kumfunga kwa mara ya kwanza bingwa wa misimu minne Simba, hivyo tutahakikisha tunamfunga Yanga kwa mara ya kwanza ili tuivunje rekodi yake kwa msimu huu.”