>

MIANZINI MABINGWA WA MERIDIAN BET STREET SOCCER BONANZA

KLABU ya Mianzini FC kutoka Temeke Jijini Dar es Salaam imefanikiwa kuibuka Mabingwa wa Meridian Bet Street Soccer Bonanza yaliyofanyika Desemba 18 mwaka huu kwenye viwanja vya Mwembeyanga.

Mianzini walitwaa ubingwa huo baada ya kuwachapa TP City FC kwa mikwaju 4-3 ya Penalti baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika kwa matokeo ya 0-0 kwenye bonanza lililoshirikisha timu nne.

 

Mianzini waliwachapa Chang’ombe Polisi FC kwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza na kutinga fainali. TP City waliwaburuza Young Boys kwa mabao 2-0. Mshindi wa tatu aliibuka Chang’ombe baada ya kushinda 4-1 mbele ya Young Boys.

Bonanza hilo lilianza kufanyika saa tatu asubuhi na kufikia tamati saa saba mchana, huku wakazi, mashabiki na wapenda soka kutoka Temeke na maeneo jirani na viwanja vya Mwembeyanga walikuwa mashuhuda wa Kandanda hiyo.

Akizungumzia Bonanza hilo na ubingwa waliopata Nahodha wa Mianzini, Ally Mkwili alisema: “Tuwashukuru Meridian Bet kwa kuandaa Bonanza hili ambalo kwa sisi vijana ni kama fursa ambayo tunapaswa tuitumie.

“Mashindano yalikuwa magumu kutokana na kila timu kujiandaa vizuri na kutaka kuwa bingwa. Kwetu ilikuwa kama mpango wetu wa kwamba lazima tuwe mabingwa na imekuwa hivyo.”

Naye nahodha wa TP City Othman Ally (Otu), alisema: “Kushika nafasi ya pili kwenye bonanza gumu kama hili ni fahari kwetu kwa sababu kila timu iliyoshiriki hapa ilikuwa inahitaji kucheza fainali.

“Niwapongeze wachezaji wenzangu kwa kazi nzuri waliyofanya, lakini kubwa niwapongeze Meridian Bet kwa kuandaa bonanza hili. Wasiishie hapa iwe mwendelezo, kuwakutanisha vijana kama hivi inakuwa jambo nzuri,”.

Twaha Mohammed kutoka Idara ya Masoko ya Meridian Bet naye alizungumza baada ya mashindano hayo kumalizika na kutoa zawadi zote kwa washindi na timu shiriki alisema:“Lengo limetimia kwetu sisi Meridian Bet, tuliandaa hili bonanza sababu kubwa ni kujitangaza kwa watu na kudumisha umoja kwa wateja wetu, lakini pia kurudisha kidogo chetu kwa vijana.

“Tulitoa fursa kwa wachezaji hawa vijana kucheza na kuonyesha vipaji vyao na vimeonekana. Niwaombe kuendelea kutuunga mkono na kuisapoti kampuni yetu.

“Mwaka 2022 utakuwa ni bora zaidi kwao, kwa sababu kuna mambo mazuri yanakuja, hasa haya mabonanza yatakuwa yanafanyika kila mwezi.”

Bingwa wa bonanza hilo alizawadiwa jezi seti mipira, na kombe, mshindi wa pili alipata jezi na mpira, huku mshindi watatu na wanne wakiondoka na jezi.