UONGOZI wa Simba umeweka wazi kwamba wao kipaumbele chao namba moja ni kazi tu uwanjani ili kupata matokeo chanya na hawana muda wa kushindana na wale wanaoongeaongea.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa wapo kwenye ligi kwa malengo makubwa ya kuweza kutetea ubingwa waliotwaa msimu uliopita na hilo linawezekana.
“Sisi hapa kwetu ni kazi tu na hatuna muda wa kuanza kubishana na wale ambao wanaongea juu yetu, ukianza kwenye upande wa kikosi pamoja na mchezaji mmojammoja kila mmoja yupo vizuri na anahitaji kutimiza majukumu yake.
“Tulichukua taji msimu uliopita na sasa tupo kwenye msimu mpya jambo pekee tunaloendelea kufanya ni kuendelea pale ambapo tuliishia kwa kupambana zaidi kupata kile ambacho tunakitana nacho ni ubingwa hakuna kingine,”amesema Mangungu.
Kikosi cha Simba kipo chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco ambaye alichukua mikoba ya Didier Gomes aliyeomba kuondoka hapo Oktoba 26.
Desemba 11, Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-0 Yanga ambapo tambo zilikuwa zakutosha kabla ya mchezo na baada ya dakika 90 wakagawana pointi mojamoja.