LICHA ya mafanikio makubwa ya upasuaji wa goti aliofanyiwa kiungo Mburkinabe wa Yanga, Yacouba Songne, imeelezwa kuwa kiungo huyo yupo hatarini kukosa michezo iliyosalia ya msimu huu kutokana na kuuguza jeraha hilo.
Yacouba alipata majeraha hayo ya goti kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ambapo upasuaji wake ulifanyika Novemba 11, mwaka huu.
Yacouba tayari amerejea nchini baada ya upasuaji huo uliofanyika nchini Tunisia na sasa anaendelea na taratibu nyingine za kusaidia uponaji wa jeraha hilo kabla ya kuanza mazoezi mepesi.
Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe,amesema kuwa hali ya kikosi ipo salama na kila kitu kinakwenda sawa kwa ajili ya msimu wa 2021/22 ila ukubwa wa jeraha la Yacouba unaweza kumfanya akakosekana msimu mzima.
“Tunashukuru hali ya maandalizi ya kikosi chetu kuelekea mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza ni nzuri, ambapo kikosi kipo kambini kuendelea na programu.
“Kuhusu hali za majeruhi, mpaka sasa majeruhi wote wamepona na wanaendelea na mazoezi ya pamoja na timu isipokuwa Yacouba ambaye amerejea nchini hivi karibuni akitokea Tunisia alipofanyiwa upasuaji wa goti, licha ya kwamba anaendelea vizuri lakini kutokana na ukubwa wa jeraha alilopata anaweza kukosekana kwa msimu mzima.”
Chanzo:Championi