YANGA imedhamiria kuwafunga kwa mara pili watani wao Simba, ni baada ya kumpumzisha kwa makusudi kiungo wao mkabaji, Mkongomani Yannick Bangala katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mchezo ujao wa ligi wa Yanga watacheza dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya ambao Bangala atakuwepo jukwaani akiutazama mchezo huo.
Dabi hiyo inatarajiwa kupigwa Desemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii uliozikutanisha timu hizo, Yanga ilifanikiwa kuwafunga Simba bao 1-0 likifungwa na
Mkongomani, Fiston Mayele.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, uongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo wamefikia makubaliano ya kutomtumia kiungo huyo kutokana na kufikisha kadi mbili za njano.
Bosi huyo alisema kuwa, kikubwa wanahofia kiungo huyo kufikisha kadi tatu za njano ambazo zitamfanya aukose mchezo ujao dhidi ya Simba ambao ni muhimu kwao.
Aliongeza kuwa wanafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza, lakini kiungo huyo atapumzishwa na Mkongomani, Mukoko Tonombe atachukua nafasi yake.
“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo wetu wa dabi ambao ni lazima tupate ushindi, kwanza pointi na pili
ni rekodi itakayowapa heshima mashabiki wetu.
“Tukielekea katika mchezo huo, kuna baadhi vitu muhimu ni lazima tuchukue tahadhari kati ya hizo ni kuwapumzisha wachezaji muhimu wenye kadi mbili katika mchezo wetu ujao wa ligi dhidi ya Mbeya Kwanza.
“Kati ya wachezaji wenye kadi mbili za njano ni Bangala ambaye tayari benchi la ufundi na viongozi wamekutana
kuzungumza hilo na kufikia muafaka wa kumpumzisha kwa hofu ya kupata ya tatu na kukosa mchezo ujao wa
dabi dhidi ya Simba,” alisema bosi huyo.Alipotafutwa Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.