KIVUMBI kinazidi kuwaka kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo kwa msimu huu mpya wa 2021/22 unaoyesha kwamba sio wa kitoto.
Wakati ligi ikizidi kuwa ni moto waamuzi wamekuwa ni pasua kichwa kwa kuonekana wakifanya maamuzi ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wengi jambo ambalo linaua ile ladha ya ushindani.
Makosa yapo lakini haina maana kwamba yawe yanajirudia mara kwa mara hii naona kwamba haipo sawa nina amini kwamba waamuzi wana uwezo mkubwa na wanaweza kufanya kazi kwa umakini tena wa hali ya juu.
Kwa upande wa matokeo ambayo yanapatikana ni suala la wale wachezaji ambao wameweza kusajiliwa pamoja na kuongezewa mikataba kwenye timu zao ambazo wapo kwa wakati huu.
Wale ambao walifanya usajili kwa umakini na kwa kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi wameweza kufanya kile ambacho kilikuwa kinahitajika.
Kutokana na maandalizi pamoja na usajili ninaweza kusema ni ngumu kuamini kwamba ushindani utakuwa mdogo hilo sioni kwa msimu huu.
Itapendeza ushindani ukiendelea mpaka mwisho wa ligi kwa kuwa kila mmoja anahitaji kuona timu inapata matokeo chanya. Matokeo mazuri yanatafutwa kwa kufanya kazi na kufanya maandalizi mazuri.
Timu zote ambazo zimefanya usajili kwa mapendekezo yao binafsi wakati wa kujua masuala hayo ni sasa. Mchezo wa mpira hauhitaji mambo mengi zaidi ya vitendo na data ambazo zinaongea ukweli muda wote.
Timu zote zinatumia dakika 90 kuweza kupata maamuzi ya kile ambacho walikifanya yule atakayetumia makosa ya mpinzani wake huonekana ni mshindi na hicho ndicho ambacho mashabiki wanahitaji.
Kama mchezaji alisajiliwa kwa presha ama shinikizo kwa sasa ni muda wa kila kitu kuwa wazi.
Ipo wazi kwamba kuna wale wachezaji ambao walipata nafasi ya kusajiliwa ndani ya timu mbalimbali hawakuwa na nafasi kwenye timu zao mpaka msimu unaisha wapo wengine walikuwa wanahitajika kwenye timu ila tatizo ikawa ni mkwanja.
Kwa viongozi wa timu pia ni somo kwamba mpira wa sasa unahitaji fedha na uwekezaji mkubwa hivyo wanajukumu la kuongeza vyanzo vyao vya mapato ili kuweza kubaki na wachezaji ambao wanawahitaji pale msimu unapokwisha.
Tukiachana na timu, mchezaji kwa sasa ana kazi ya kutimiza majukumu yake kwa usahihi ndani ya uwanja ili kurejesha imani kwa mashabiki ambao wanawaamini.
Kwa kuwa maisha ya soka lazima yaendelee mchezaji mmoja kuondoka na kwenda katika timu nyingine hilo halizuiliwi.
Kwa kuwa tayari ligi imeshaanza basi ni muhimu kuona kwamba kila mmoja anapaswa kutimiza majukumu yake ipasavyo hii itafanya ushindani kuwa imara na bora.
Rai yangu kubwa hasa kwa waamuzi ambao ni sehemu ya mchezo na mafanikio ya mpira wetu wanapaswa wasipepese macho katika kazi yao ndani ya uwanja.
Kufanya kwao vizuri ni hazina kwa ajili ya bingwa ambaye atapatikana hapo baadaye kwa kuwa ana kazi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa hivyo atakwenda kufanya vema kwa kuwa hajabebwa.
Ipo wazi kwamba, waamuzi ni binadamu na makosa yapo lakini haipaswi iwe kila siku wao wanabebeshwa zigo la lawama kila baada ya mchezo kuiisha hii haifai.
Kusimamia kwao majukumu ambayo wamepewa kwa uzuri kutaongeza ule ushindani kufanya kila timu kupata ushindi baada ya dakika 90 bila kuwa na sehemu ya kushusha lawama.
Kila timu kwa sasa inahitaji pointi tatu muhimu hilo lipo wazi na kwa namna mambo yanavyokwenda hivi ndivyo inatakiwa kuwa mpaka mwisho wa msimu.
Bado kwa sasa kumekuwa na malalamiko ambayo yanatolewa hilo huwezi kukwepa lakini ikiwa waamuzi wataamua kufanya kweli inawezekana. Kufuata sheria 17 na kufanya maamuzi sahihi ni tiba tosha kwa haya malalamiko ambayo yamekuwa yakiskika kutoka kwa viongozi.
Tunataka kuona kila timu inafanya maajabu na kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote ambazo watacheza iwe nyumbani ama ugenini muhimu kupambana kupata matokeo.