YANGA HAWANA HABARI NA ISHU YA KOCHA SIMBA

WAKATI wengi wakisema ujio wa kocha mpya wa Simba, Pablo Franco utakuwa ni changamoto kubwa kwa Yanga kutokana na wasifu mkubwa alionao, lakini uongozi wa Yanga wala hauna presha wakimuamini kocha wao, Nasreddine Nabi.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu Simba imtangaze kocha huyo raia wa Hispania aliyekuja kuchukua nafasi ya Mfaransa, Didier Gomes na jana Novemba 10 aliwasili Dar kwa ajili ya kuanza kufanya kazi kwenye benchi la ufundi.

Akizungumza na Spoti Xtra, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Injinia Hersi Said alisema kuwa wana matumaini makubwa na kocha wao Nabi, hivyo hawawezi kukaa kumfikiria
Muhispania huyo.

 

Aliongeza kuwa wanaamini ubora na mbinu za kocha Nabi ambazo zitaipa mafanikio msimu huu na ujao katika kutwaa makombe.

 

“Huu siyo muda wa kukaa kumfikiria kocha wa timu pinzani na badala yake akili na nguvu zetu tunazielekeza katika timu kufanya vema.

 

“Ukaribu wetu na La Liga, Sevilla siyo sababu ya sisi kuanza kumfuatilia kocha huyo wa Simba aliyekuwa anaifundisha Getafe inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania.

 

Hiyo siyo kazi yetu, hilo lipo kwa kocha ambaye naye ngumu kuanza kumfuatilia kwa hivi sasa na badala yake nguvu na akili zake amezielekeza katika michezo ijayo ya ligi,” alisema Hersi