BEKI wa kimataifa wa Simba, raia wa DR Congo, Enock Inonga kabla ya kwenda kuungana na kikosi cha timu yake ya Taifa ya DR Congo, alilazimika kumuomba radhi Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez na viongozi wengine, kufuatia kosa la kadi nyekundu aliyopata dhidi ya Coastal Union.
Inonga kwa sasa yupo kambini na timu yake ya Taifa ya DR Congo, kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa kufunzu Kombe la Dunia dhidi ya Taifa Stars utakaopigwa leo Uwanja wa Mkapa jijini Dar.
Chanzo chetu kutoka Simba, kimeliambia Championi Jumatano kuwa, kabla ya Inonga kuondoka kambini alilazimika kuwaomba upya radhi wachezaji na benchi zima la ufundi lililokuwa sambamba na uongozi wa timu hiyo chini ya CEO wake Barbara, huku akiahidi kutofanya tena kosa kama hilo.
“Wakati Inonga akiaga kwa ajili ya kujiunga na kikosi chake cha timu ya taifa, alilazimika kuomba radhi kwa mara nyingine kwa wachezaji na benchi la ufundi, huku akiahidi kutoruhusu hasira za aina hiyo kutokea kiasi cha kusababisha kuigharimu timu kwenye mchezo dhidi ya Namungo baada ya kukosekana.
“Uongozi kwa pamoja na benchi la ufundi ulimsamehe, huku ukimtaka kubadilika kweli na kuwa mfano kwa wenzake na endapo siku nyingine atafanya hivyo basi watalazimika kumfungia na kumkata mshahara kabisa,” kilisema chanzo hicho.