>

TAIFA STARS MATUMAINI KAMA YOTE KUFUZU KOMBE LA DUNIA

HESABU kubwa kwa sasa kwa Kim Poulsen ambaye ni Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ni kuona namna gani timu hiyo itafanikiwa kufuzu Kombe la Dunia.

Novemba 11, Stars itakuwa na kazi mbele ya DR Congo mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Spoti Xtra limezungumza na Poulsen ambaye anafunguka mipango namna hii:-

“Wachezaji wapo vizuri na kila mmoja anatambua kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya na ipo wazi kuwa ni kazi kubwa kwani kupambana na timu ambayo inahitaji ushindi pia ni jambo gumu.

“Siku ambazo tutaanza mazoezi itakuwa ni muhimu kwa kila mchezaji kupata kile ambacho tutakuwa tunakitoa hasa maelekezo na mbinu kwa ajili ya mechi zetu ambazo tutacheza kwa ajili ya kutafuta ushindi.

Safu yako ya ushambuliaji unaitazamaje?

“Kweli ni kitu muhimu kwenye timu lakini kila mchezaji ana umuhimu kwenye nafasi yake na hakuna ambaye anapaswa kufunga pekee bali timu nzima.

“Ili uweze kushinda ni lazima ufunge hilo ndilo ambalo tunalihitaji na kwa namna ambavyo tunawapa maelekezo vijana na vile ambavyo wanayafanyia kazi ninaona kwamba kuna mabadiliko ambayo yanakuja na tutafanya vizuri.

Makosa ambayo yanafanywa na wachezaji wako je?

“Ni mpira ambao ni sehemu ya makosa hivyo paele ambapo wanakosea tunapata muda wa kurekebisha makosa na kuweza kuwa imara kwa ajili ya mechi zetu zijazo. Kila siku huwa tunapata muda wa kuzungumza na wachezaji ili kujua wapi tumekosea na tuwe imara kwa namna gani.

Sura mpya ndani ya timu je?

“Hii ni timu ya kila mmoja hivyo wale ambao wanafanya vizuri wanaingia kwenye kikosi kwa ajili ya maandalizi. Ninapenda kuona wale ambao ninawapa nafasi wanatimiza majukumu vizuri kwa sababu kinachotafutwa ni ushindi na sio sura mpya kwenye kikosi.

Huwa unawafuatilia wachezaji kwenye ligi?

“Ipo wazi huwa ninatazama michezo ya ligi na mechi mbalimbali ninatazama ninaona namna wachezaji wanavyofanya vizuri.

“Wapo wengine ambao nilikuwa nao kwenye timu baadaye wakapata usajili kwenye timu nyingine hilo naona ni jambo zuri kwangu na kwa ajili yao inaonesha kuna kitu kiliwafanya wakaonekana na leo hii wanapata matunda ya kile ambacho walikuwa wanakifanya.

Mshambuliaji Kibu ni moja ya hao ila hajafunga unadhani kwa nini?

“Kufunga wakati mwingine unaweza kusema ni bahati. Naona Kibu, (Dennis) ni moja ya washambuliaji wazuri ambao wakipewa muda watafanya mengi makubwa.

“Unajua kupata nafasi kwenye timu ambayo unacheza kwa sasa kisha ukapata nafasi ya kutengeneza maana yake ni kwamba kuna maendeleo ambayo yapo na akifanikiwa kupata anachokitaka basi atafanya vizuri na wengine wengi naona wanakuja vizuri.

Malengo makubwa kwa sasa yapo kwenye nini?

“Mechi zetu ambazo tutacheza tunahitaji ushindi licha ya kwamba tunaongoza kundi tunajua kazi inaendelea na ili kuweza kufuzu Kombe la Dunia tunapaswa kupata matokeo mazuri na kwa kuwa mchezo ujao tutakuwa nyumbani hawa vijana ambao nimewaita nina imani nao na tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu,” alisema Poulsen.