Home Sports DAKIKA 450 ZA JASHO JINGI SIMBA

DAKIKA 450 ZA JASHO JINGI SIMBA

IKIWA kwa sasa ipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hitimana Thiery na msaidizi wake Seleman Matola timu ya Simba imekamilisha dakika 450 za jasho jingi uwanjani huku ikiwa kwenye mwendo wa kushinda bao mojamoja kwenye mechi zake ilizoshinda.

Simba ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na msimu wa 2021/22 wanapata upinzani wa maana kutoka kwa watani zao wa jadi Yanga ambao hawajaacha pointi hata moja kwenye mechi tano ambazo wamecheza wakiwa wamejikusanyia pointi 15.Mabingwa hao watetezi wenyewe kibindoni wamekusanya jumla ya pointi 11 ikiwa imeachwa kwa jumla ya pointi nne na Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.

Muziki wao waliufungua kwa kucheza mbele ya Biashara United ya Mara ilikuwa Uwanja wa Karume,Mara na dakika 90 zilikamilika ubao ukasoma Biashara United 0-0 Simba.

Kete ya pili ilianguka Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ukasoma Dodoma Jiji 0-1 Simba kisha kituo kilichofuata ilikuwa Uwanja wa Mkapa, Simba 1-0 Polisi Tanzania kisha wakabanwa mbavu kwa ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 0-0 Coastal Union.

Dakika 450 zilikamilishwa kwenye mechi ya tano mbele ya Namungo FC ambapo ngoma ilikuwa nzito mpaka dakika ya 90 baada ya jasho jingi kuvuja Simba ikapata bao la ushindi kupitia kwa Meddie Kagere akitumia pasi ya Mohamed Hussein.

Tabu kubwa kwa Simba inaonekana kwenye safu ya ushambuliaji ambapo katika mechi tano imeambulia mabao matatu na ni mshambuliaji Kagere mwenye mabao mawili huku Rally Bwalya ambaye ni kiungo akiwa na bao moja alifunga mbele ya Polisi Tanzania kwa penalti.

Kipa wao namba moja Aishi Manula amezidi kuwa imara kwenye lango kwa kuwa katika mechi zake tano hajaruhusu bao huku safu yake ya ulinzi ikifanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Shomari Kapombe, Joash Onyango, Kened Juma na Henock Inonga.

Previous articleVARANE KUZIKOSA MAN CITY, CHELSEA, ARSENAL
Next articleKIKOSI BORA CHA HAJI MANARA,SIMBA ‘OUT’